Nafasi Ya Matangazo

June 01, 2024












Katibu Tawala wa mkoa wa Singida Dkt. Fatuma Mganga, amewaagiza Maafisa Michezo kutoka Halmashauri Saba za mkoa huo wahakikishe wanachagua wanafunzi wenye vipaji na vipawa ambao wataenda kuuwakilisha mkoa kwenye mashindano ya Kitaifa ya Umoja wa Michezo na Taalum kwa wanafunzi wa shule za msingi (UMITASHUMTA) ambayo yatafanyika Kitaifa hivi karibuni Mkoani Tabora.

Katibu Tawala huyo wa mkoa ametoa maagizo hayo (tarehe 31 Mei, 2024) wakati anafunga mashindano UMITASHUMTA yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Mwenge kwa kushirikisha wanafunzi zaidi ya 700 kutoka Halmashauri za Mkoa wa Singida.

Dkt. Fatuma Mganga amesema anaimani kubwa uchaguzi wa wanafunzi watakaowakilisha mkoa kwenye mashindano hayo watarudi na makombe ya kutosha katika kila aina ya mchezo.

Amesisitiza maandalizi kwa wanafunzi hao yawe bora ikiwemo matumizi ya vifaa na zana za kisasa ili mkoa ushike nafasi ya kwanza kwenye mashindano hayo.

Katibu Tawala huyo pia amewataka Maafisa michezo wa Halmashauri kutumia kauli mbiu ya mwaka huu ya UMITASHUMTA kupitia fani ya uimbaji (kwaya) kutangaza mafanikio ya utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa katika awamu ya sita ikiwemo shule (majengo ya madarasa), hospitali, miundombinu ya barabara, kilimo, maji na sekta mbalimbali zinazotekelezwa mkoani Singida.

Aidha, kwa mwaka 2023 mkoa wa Singida ulishika nafasi ya Tisa kitaifa na kutoa wanafunzi 12 waliounda Timu ya Taifa.

Naye Afisa Michezo, Utamaduni na Sanaa wa Mkoa wa Singida, Amani Mwaipaja, amesema mashindano hayo mwaka huu yalianza kufanyika ngazi ya shule, kata, Wilaya na sasa mkoa kwa kushindania michezo saba ambayo ni mpira wa miguu, netboli, mpira wa mikono, mpira wa wavu, mpira wa kikapu na riadha.

Amesema kumekuwa na Halmashauri zenye wanafunzi wenye mahitaji maalum ambao pia walishirikishwa kwenye mashindano kutoka Manispaa ya Singida kulikuwa na timu ya mpira wa miguu kwa wanafunzi viziwi, Ikungi na Iramba kulikuwa na wanafunzi wenye uoni hafifu na ualbino.

Mwaipaja amesema mashindano haya ambayo yaliwashirikisha jumla ya wanafunzi 732 kutoka Halmashauri za Wilaya ya Iramba, Ikungi, Singida DC, Mkalama, Manyoni, Itigi na Manispaa ya Singida yalianza Mei 28, 2024 na kuhitimishwa Mei 31, mwaka huu ambapo waliweka kambi katika Shule ya Sekondari Mwenge iliyopo Manispaa ya Singida.

Amesema baada ya mashindano haya kuliundwa timu ya mkoa iliyowajumuisha wanafunzi 120 pamoja na walimu timu itakayoandaliwa kwa ajili ya mashindano ya kitaifa yatakayofanyika katika Mkoa wa Tabora.

Mwaipaja akizungumza maendeleo ya michezo ya UMITASHUMTA na UMISSETA kwa mwaka 2023, amesema Mkoa wa Singida ulipata mafanikio makubwa ikiwamo kupata kombe la mshindi wa pili mpira wa miguu na Netball kwa wasichana.

Mafanikio mengine Mkoa ulipata mwanafunzi mtunzi bora wa nyimbo za kizazi kipya, kupata medali 4 za shaba kutoka kwa wanafunzi walioenda kushiriki mbio za nyika mashindano ya dunia yaliyofanyika jijini Nairobi nchini Kenya.

Mwaipaja amesema mafanikio mengine yaliyopatikana ni medali ya shaba ya mwanariadha Zahara Ramadhani kwenye mashindano ya taifa ya Ladies first yanayoratibiwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Chama cha Riadha Tanzania na Shirika la JAICA kutoka Japan.

“Tunamshukuru Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwezesha michezo hii na kutoa fursa kwa wanafunzi kukutana na kufurahi pamoja, hali hii inaakisi upendo wa dhati wa Rais kwa Watanzania," amesema Mwaipaja.
Posted by MROKI On Saturday, June 01, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo