Nafasi Ya Matangazo

June 01, 2024

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mh. Dkt. Dotto Mashaka Biteko amelipongeza Jiji la Dodoma kwa mikakati ya kuboresha na kukuza Elimu Dodoma Jiji na pia amempongeza Mbunge Anthony Mavunde kwa ubunifu wa kuandaa mkutano, ambao ameufungua leo Jijini Dodoma,wa pamoja wa wakuu wa Shule za Msingi & Sekondari na Waratibu Elimu Kata kwa lengo la kujadiliana changamoto za mhula uliopita na kujipanga na mhula ujao kuanzia mwezi Julai 2024.

Aidha Dkt. Biteko ametumia fursa hiyo kuwapongeza walimu wote nchini kwa kazi nzuri wanayofanya katika kujenga kizazi bora kijacho chenye nidhamu,maadili na kujitambua.

"Kama tunataka kujenga taifa lenye ustaarabu, kustahimiliana na lenye amani, mahali pekee pa kuwekeza ni kwenye elimu, mataifa yote
yaliyoendelea uwekezaji wake mkubwa upo kwenye elimu"Alisema Dkt. Biteko

Naye Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Mh. Prof. Adolph Mkenda amepongeza hatua hizi za kuwaongezea morali wa kufanya kazi walimu kwa kukutana pamoja na viongozi kujadiliana changamoto za kwenye sekta ya Elimu na kuongeza kuwa Serikali inajenga vyuo 64 vya VETA nchi nzima, kampasi za vyuo vikuu kwenye mikoa karibu yote nchini ili kuboresha upatikanaji wa elimu kwenye maeneo jirani.

Akitoa maelezo ya awali,Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mh. Rosemary Senyamule amempongeza Mh Rais Dkt. Samia S. Hassan kwa uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya elimu Mkoani Dodoma na kupelekea ongezeko kubwa la ufaulu mkoani Dodoma kwa miaka ya hivi karibuni.

Akizungumza madhumuni ya mkutano huo,Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh.Anthony Mavunde amesema lengo la kukutana na walimu hawa ni kujadiliana mafanikio na changamoto za mhula  uliopita na kujipanga na mhula ujao ili tuweze kulitendeahaki jiji letu la Dodoma kwenye sekta ya elimu kwa kuweka mikakati kabambe ya kuboresha sekta.

Katika mkutano huo Mbunge Mavunde amekabidhi *photocopiers* *10* kubwa kwa lengo la kuchapisha mitihani na kuwapunguzia mzigo wazazi wa watoto wa Dodoma Jiji kuchangia fedha za mitihani ya majaribio ya kila wiki.
Posted by MROKI On Saturday, June 01, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo