Nafasi Ya Matangazo

May 23, 2024

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana, Lucas Malia ya Ruangwa Mkoani Lindi wakifuatilia kipindi cha Mwaswali bungeni jijini Dodoma, Mei 23, 2024. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana, Lucas Malia ya Ruangwa, kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma, Mei 23, 2024. Wanafunzi hao walikwenda bungeni kujifunza kwa mwaliko wa Mbunge wa Ruangwa na Waziri Mkuu. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akijibu maswali, bungeni jijini Dodoma, Mei 23, 2024. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana, Lucas Malia ya Ruangwa Mkoani Lindi wakifuatilia kipindi cha Mwaswali bungeni jijini Dodoma, Mei 23, 2024. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
**************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wazazi na walezi wafuatilie mienendo ya watoto wao waendapo shuleni ikiwemo na mahudhurio na masomo yao darasani.

“Serikali inaendelea kuimarisha mahudhurio ya watoto shuleni kwa kuzungumza na wazazi ili kuhakikisha kila mzazi anasimamia mahudhurio ya mtoto wake, kwenda shule, kuingia darasani, lakini anaporudi nyumbani, mzazi afuatilie mwenendo wa masomo ya mtoto huyo ili ajiridhishe kama kweli mtoto alikwenda shuleni.” 

Ametoa wito huo Bungeni leo (Alhamisi, Mei 23, 2024) wakati akijibu swali la Mbunge wa Sikonge, Joseph Kakunda kwenye kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu ambaye alihoji Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha wanafunzi wanaoanza masomo wanamaliza wote shule ukiacha wale ambao hufariki dunia. 

Katika ngazi ya shule za sekondari, Waziri Mkuu amesema: “Tunaimarisha ujenzi wa mabweni na hosteli kwaajili ya wanafunzi wa kike na wa kiume ili wasome palepale, walale pale, wacheze pale lakini pia usimamizi wa maadili yao uweze kuimarika.”

Amesema maelekezo yalikwishatolewa kwenye Halmashauri zote za Wilaya kwani ndizo zinasimamia shule za msingi na sekondari na kwenye ngazi za mikoa ili wafanye ufuatiliaji shuleni. 

“Pia tumeimarisha taasisi yetu ya Uthibiti Ubora ambayo moja ya majukumu yake ni kuhoji idadi ya wanafunzi waliosajiliwa, waliopo darasani na wanatakiwa wahoji ni kwa nini wengine hawapo kulingana na usajili uliopo.”

“Tunaamini kupitia hatua hizi, utoro utapungua na tutaanza kuona wanafunzi waliosajiliwa wanafikia asilimia 95 hadi 98 ya wanaomaliza.” 

Wakati huohuo, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha kuwa wanafunzi walioacha masomo kwa sababu mbalimbali wanarejeshwa shuleni ili waweze kutimiza ndoto zao.

“Ninampongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kipindi chake cha uongozi alielekeza wanafunzi wa kike waliochishwa masomo warudi shuleni ili waweze kutimiza ndoto zao.” 

Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Asia Abdukarimu Hamlanga, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kulifanyia kazi suala hilo kupitia maboresho ya Sera ya Elimu yanayofanyika sasa. 

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewashukuru wananchi wanaoishi kandokando ya maeneo yaliyohifadhiwa kisheria na kwamba Serikali inatambua mchango walionao katika kulinda maeneo hayo.

Amesema Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wananchi wanaoishi kwenye maeneo hayo, pia inaweka alama katika mipaka iliyowekwa kisheria. “Tunaendelea kutoa elimu kwa kushirikiana na Kamati za Mazingira za kila kijiji juu ya uhifadhi, ulinzi wa mipaka na tunawapa nguvu ya kusimamia maeneo hayo.”

“Nitoe wito kwa wahifadhi wote wanaolinda maeneo yaliyohifadhiwa, wajenge mshikamano na wananchi wanaoishi jirani na maeneo hayo kwa kujenga tabia ya kufanya mazungumzo na Serikali za vijiji zilizoko kwenye maeneo hayo,” amesisitiza.

Alikuwa akijibu swali la Mbunge Viti Maalum, Stella Simon Fiyao ambaye alitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu kwa umma ili wananchi wote wawe sehemu ya kulinda maeneo ya hifadhi na kuepusha migogoro na wahifadhi
Posted by MROKI On Thursday, May 23, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo