Nafasi Ya Matangazo

May 15, 2024

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza na Balozi wa Tanzania nchini Comoro, 
Mhe. Saidi Yakubu  wakati Balozi huyo mpya wa Tanzania nchini Comoro  alipofika kumuaga Ikulu Jijini Dar es salaam.
Balozi mpya wa Tanzania nchini Comoro Mhe. Saidi Yakubu

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi mpya wa Tanzania nchini Comoro Mhe. Saidi Yakubu aliyefika kumuaga Ikulu Jijini Dar es salaam.
 
Akizungumza na Balozi huyo, Makamu wa Rais amemtaka kusimamia sera ya diplomasia ya uchumi na kutafuta maeneo mapya ya ushirikiano kwa kuibua fursa zaidi za kiuchumi. Amesema dhamira ya Tanzania ni kuendeleza na kuimarisha ushirikiano mzuri uliyodumu kwa muda mrefu na Taifa la Comoro.
 
Pia Makamu wa Rais amemuagiza Balozi Yakubu kufuatilia utekelezaji wa mikataba mbalimbali ya ushirikiano iliyopo katika sekta mbalimbali ili kufungua fursa za kiuchumi kwa pande zote mbili.
 
Halikadhalika amemsihi Balozi huyo kuwa na nyenzo muhimu za kazi zitakazomuwezesha kufahamu vema vipaumbele vya taifa kama vile Dira ya Taifa, Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano, Ilani, Sera ya Mambo ya Nje, pamoja na takwimu sahihi na za msingi kuhusu Tanzania.
 
Amemtaka kuvutia wafanyabiashara na wawekezaji pamoja na kuongeza zaidi thamani ya biashara baina ya mataifa haya mawili ambapo kwa sasa imefikia dola za marekani milioni 55.
 
Pia amesema ni muhimu ubalozi kuweza kutoa taarifa juu ya masuala ya huduma za afya zinazopatikana nchini ili kuwarahisishia wananchi wa Comoro wanapohitaji matibabu. Ameongeza kwamba ni vyema kuwaunganisha Watanzania wanaoishi nchini Comoro na kuwavutia  kuwekeza nchini.
 
Kwa Upande wake Balozi Yakubu amemshuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumteua kumwakilisha nchini Comoro ambapo ameahidi kuendeleza ushirikiano uliopo na kuimarisha diplomasia ya uchumi ikiwemo kuongeza biashara baina ya mataifa haya mawili.
 
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amekutana na kufanya mazungumzo na na Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi Nchni (UNHCR) Bi. Mahoua Parum’s pamoja na Mwakilishi wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) Bi. Clara Makenya Ikulu Jijini Dar es salaam.

Mazungumzo hayo yamelenga kuongeza ushirikiano katika sekta ya mazingira hususani kuwasaidia wananchi kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.L
Posted by MROKI On Wednesday, May 15, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo