Nafasi Ya Matangazo

May 06, 2024

Mkurugenzi wa Usalama na Mazingira Wizara ya Ujenzi Eng. Kashinde Musa akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufua mafunzo kwa wafanyakazi wa mizani kanda ya ziwa yanayoendelea jijini mwanza.
Mkurugenzi wa Usalama na Mazingira Wizara ya Ujenzi Eng. Kashinde Musa (kulia) na Kaimu Meneja wa mizani wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Eng. Japhet Kivuyo wakifuatilia mafunzo kwa watumishi wapya wa mizani kanda ya ziwa yanayoendelea jijini Mwanza.
Baadhi ya watumishi wa mizani kutoka mikoa ya kanda ya ziwa wakifuatilia mafunzo ya utendaji kazi wenye weledi kwa wafanyakazi wa mizani wa mikoa sita ya kanda hiyo yanayoendelea jijini Mwanza.
Baadhi ya watumishi wa mizani kutoka mikoa ya kanda ya ziwa wakifuatilia mafunzo ya utendaji kazi wenye weledi kwa wafanyakazi wa mizani wa mikoa sita ya kanda hiyo yanayoendelea jijini Mwanza.
Mkurugenzi wa Usalama na Mazingira Wizara ya Ujenzi Eng. Kashinde Musa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wapya wa mizani wanaopata mafunzo kutoka mikoa sita ya kanda ya ziwa. 
Mkurugenzi wa Usalama na Mazingira Wizara ya Ujenzi Eng. Kashinde Musa amewaasa wafanyakazi wa mizani kujiepusha na vitendo vya rushwa ili kulinda miundombiniu ya barabara na hivyo kufanya kazi kwa tija.

Akizungumza jijini Mwanza wakati akifungua mafunzo kwa wafanyakazi wapya wa mizani kanda ya ziwa Eng. Kashinde amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua kali za kisheria kwa wote watakaobainika kujihusisha na rushwa kwa kuzidisha uzito na kusababisha barabara kuharibika kabla ya wakati uliokusudiwa.

“Serikali imewaamini na itawapa ushirikiano na mafunzo kila wakati ili mfanye kazi kwa weledi na hivyo kuleta tija kwa miundombinu ya barabara na sekta ya usafirishaji kwa ujumla”, amesema Eng. Kashinde.

Amesema Serikali inaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya barabara mpya kwa kiwango cha lami sambamba na kujenga mizani kwenye maeneo ya kimkakati ili kudhibiti uharibifu unaotokana na uzidishaji uzito wa magari na kuhakikisha barabara zinalindwa ili zidumu kwa kipindi kilichokusudiwa.

“Pasipo kudhibiti uzito barabara zetu zitaharibika mapema na hivyo kusababisha Serikali kuingia gharama kubwa za matengenezo, jambo ambalo lina athari katika kukuza uchumi wa nchi”, amesisitiza Mkurugenzi huyo wa Usalama na Mazingira Wizara ya ujenzi.
 

Mafunzo hayo yamewalenga wafanyakazi wapya wa mizani  katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara, Geita, na Kagera lengo likiwa ni kupata uelewa wa pamoja katika utekelezaji wa Sheria ya Udhibiti Uzito wa Magari ya Mwaka 2016 na Kanuni zake za mwaka 2018, taratibu za utendaji kazi kwenye mizani, maadili ya Utumishi wa Umma, elimu kuhusu vitendo vya rushwa na utoaji wa huduma bora kwa wateja.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa mizani TANROADS makao makuu Eng. Japhet Kivuyo amesisitiza umuhimu wa watumishi wa mizani kufanya kazi kwa weledi na ubunifu ili kuelimisha na kutatua changamoto zinazowakabili wasafirishaji na hivyo kuwezesha sekta ya usafirishaji nchini kuwa na tija.

“Hakikisheni mnatoa huduma bora ili wasafirishaji wa ndani na nje ya nchi wawaelewe na wafuate sheria bila shuruti na hivyo kulinda barabara zetu”, amesema Eng. Kivuyo.

Zoezi hilo la utoaji elimu linalofanywa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), ni endelevu ambapo takriban wasafirishaji 2,100 katika miji na vijiji vyenye uzalishaji mkubwa wa mizigo wamepata mafunzo hayo katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2022/2023 na 2023/2024.

 

Posted by MROKI On Monday, May 06, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo