Nafasi Ya Matangazo

April 21, 2024









Na Mwandishi wetu
Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amewataka Wananchi kufuata sheria, misingi, kanuni na taraatibu na kuachana na vitendo viovu vinavyopelekea mlundikano wa wafungwa katika magereza.

Akihutubia leo Aprili 21, 2024 katika hafla fupi ya Uwekaji Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Gereza la Wilaya ya Gairo katika Kitongoji cha Majembwe Kata ya Msingisi Wilaya ya Gairo, Mkoani Morogoro  ikiwa ni Shamrashamra za kuelekea Maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano, Mhe. Abdulla alisema kwamba ni vema Wananchi wote wakatii sheria na taratibu za nchi zilizowekwa ili kuepukana na kuishia magerezani.

"Ukitii sheria za nchi utakuwa umeepukana kuwa mteja wa magereza pia nichukue fursa hii kuipongeza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kuhakikisha inasimamia vyema Vyombo vyake vya Ulinzi na Usalama kwani tunaona wazi nchi yetu ina amani na utulivu wakutosha," Alisema Mhe. Abdulla.
 
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Daniel Sillo (Mb) alieleza kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali ilitenga Shilingi 4,569,000,000.00 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa magereza sita (6), likiwemo Gereza la Wilaya ya Gairo ambalo muda mchache umetoka kuweka Jiwe la Msingi wewe mwenyewe Mhe. Makamu wa Pili wa Rais.

"Mhe. Mgeni rasmi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kutokana na fedha hizo nilizozitaja hapo juu nipende kumshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu kwa kuendelea kuimarisha miundombinu ya mazingira ya kazi na usalama wa maeneo ya kazi kwa kuruhusu ukarabati wa magereza ya zamani na ujenzi wa magereza mapya pamoja na kuboresha makazi ya watumishi" alisema Mhe. Sillo.

Aidha, Mhe. Sillo alieleza kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikitoa maelekezo mbalimbali kuhusu utoaji wa Haki jinai, hususani kwa Vyombo vya Usalama vilivyo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa lengo la kuviongezea uwezo Vyombo hivyo kusimamia utekelezaji wa sheria na kutoa huduma bora kwa Wananchi.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali pamoja na viongozi kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wakiongozwa na Dkt. Maduhu Kazi, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Kamishna wa Jeshi la Magereza Mzee Ramadhani Nyamka, Maafisa Waandamizi, Maafisa na Askari wa vyeo mbalimbali kutoka Jeshi la Magereza.

Hata hivyo Gereza hilo la Wilaya ya Gairo litahudumia zaidi ya wafungwa 500 na kupunguza kusafirisha wafungwa kwa zaidi ya kilomita 100 pamoja mlundikano wa wafungwa katika Magereza yaliyopo katika wilaya za jirani pindi litakapokamilika.
Posted by MROKI On Sunday, April 21, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo