Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel John Nchimbi amesema kuwa CCM, chini ya Mwenyekiti wake, ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kudumisha uhusiano na urafiki wa muda mrefu kati ya Tanzania na Urusi, ukilenga kuboresha maeneo ya uwekezaji, biashara na uchumi, kwa ajili ya manufaa ya pande zote mbili.
Balozi Dk. Nchimbi amesema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Urusi nchini Tanzania, Mhe. Andrey Avetisyan, ambapo amesisitiza kuwa kuboresha maeneo ya uwekezaji, biashara na uchumi, kutaimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Serikali za nchi hizo mbili na wananchi wake na kuufanya kuwa wa moja kwa moja zaidi.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika leo Alhamis, Februari 23, 2024, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba, jijini Dar Es Salaam, pamoja na kurejea kumbukumbu za uhusiano wa muda mrefu wa Tanzania na Urusi, tangu wakati wa kupigania uhuru na baada ya uhuru, ambao mwaka huu unafikisha miaka 62, walizungumzia maeneo ambayo yanaweza kufanyiwa kazi na Serikali za nchi hizo, chini ya uongozi wa vyama vinavyoongoza nchi hizo, Chama Cha Mapinduzi na United Russia, mtawalia.
Kwa upande wake, Balozi wa Urusi nchini Tanzania, Mhe. Andrey Avetisyan, mbali ya kumpongeza na kumtakia kila la heri Balozi Dk. Nchimbi kwa kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM, ameelezea uhusiano wa muda mrefu wa Urusi kwa Tanzania na nchi za Afrika, tangu wakati wa kupigania uhuru na baada ya uhuru, ambapo ilikuwa mojawapo ya nchi za mwanzo kuitambua Tanganyika huru, akisisitiza kuwa chini ya uongozi wa Rais Vladimir Vladimirovich Putin, na mazingira mazuri ya uwekezaji, biashara na uchumi ya Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Urusi iko tayari kuendelea kuenzi na kuimarisha uhusiano utakaonufaisha pande zote mbili.
0 comments:
Post a Comment