Nafasi Ya Matangazo

February 29, 2024

Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi,Uenezi na Mafunzo CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis,akizungumza na Wanachama wa Jumuiya ya Wamasai waishio Zanzibar katika bustani ya Forodhani Unguja.
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi,Uenezi na Mafunzo CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis,akiwa na Viongozi wa kimila wa jamii ya wamasai mara baada ya kufanya kikao huko Forodhani Unguja.
 ***************
Na Mwandishi wetu, Zanzibar
CHAMA Cha Mapinduzi(CCM)Zanzibar,kimewataka baadhi ya Wananchi kuacha tabia za kuwabagua kwa misingi ya kikabila na kiutamaduni watu wanaotoka katika jamii ya kimasai nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi,Uenezi na Mafunzo CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis, wakati akizungumza na Jumuiya ya Wamasai waishio Zanzibar huko Forodhani Jijini Zanzibar.

Mbeto,alisema jamii ya wamasai ni miongoni mwa makabila 120 yaliyopo Tanzania wenye haki ya kuishi popote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufuata sheria zote za nchi.

Alieleza kuwa sio sahihi baadhi ya wananchi kutumia matukio yaliyotokea hivi karibuni ya ugomvi wa baadhi ya wamasai na maafisa wa Manispaa ya Mjini Zanzibar kuwa ni kigezo cha kuwatenga na kuwakosesha haki zao za msingi,kwani changamoto hiyo imetatuliwa na vyombo vya ulinzi na usalama.

Katika maelezo yake,Katibu huyo wa NEC Mbeto,anasema baada ya changamoto hiyo kumejitokeza baadhi ya wananchi na wengine ni watumishi wa umma wamekuwa wakiwakosesha jamii hiyo huduma mbalimbali za kijamii tabia inayotakiwa kukemewa vikali.

“ Chama Cha Mapinduzi kinapiga vita vitendo vya ubaguzi hasa vyenye viashiria vya ukabila kwani madhara yake ni makubwa katika maisha ya kila siku ya jamii zetu na inaweza kusababisha migogoro ya kikabila.

Leo itokee wamasai nao huko kwao Arusha na maeneo mengine ya Tanzania bara waanze kuwabagua na kuwakosesha huduma za kijamii watu wenye asili ya Zanzibar je tutajisikiaje,hatuhitaji kufikia huko kwani sisi ni wamoja na tunatakiwa kuishi kwa upendo na mshikamano.”alisisitiza Mbeto na kuongeza kuwa ikitokea mtu mmoja au kundi wamefanya uhalifu basi wachukuliwe hao sio jamii yao nzima.

Alisema Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 pamoja na Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977, zote zinaelekeza haki na utu wa kila mtu kuheshimiwa hivyo jamii ya wamasai wasivunjike moyo na waendelee kuishi kwa kulinda amani na utulivu wa nchi.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar italinda haki zao mbalimbali zikiwemo za utamaduni kwani kila jamii ina utamaduni wake utaotakiwa kuthaminiwa kisheria.

Kupitia kikao hicho Mbeto, aliwahakikishia kuwa wamasai wenye sifa za kuwa Wanachama wanakaribishwa kujiunga na CCM na wana haki ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kuanzia ngazi za Mashina hadi Taifa.

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo kanda ya Mjini Mathayo Joseph,alisema lengo la kikao hicho ni kutafuta suluhu juu ya changamoto zinazowakabili katika utekelezaji utekelezaji wa majukumu yao.

Alisema kuna baadhi ya maeneo wanapata wakati mgumu kwa kunyanganywa vifaa vyao vya kitamaduni vikiwemo sime na rungu huku wakitolewa kauli zisizofaa zinazowatuhumu kuwa ni wahalifu.

“Miaka yote tumeishi Zanzibar kwa amani na utulivu hatujawahi kuhusishwa wala kukamatwa kwa tukio lolote la kihalifu na mmasai mmoja akifanya kosa ahukumiwe yeye  kwani hajatumwa na jamii ya wamasai.”, alifafanua Joseph.

Naye Mwanachama wa Jumuiya hiyo Joseph Olelei,alisema kwa sasa kuna maeneo wanazuiwa kufanya biashara hata kwa wale wanaofanya kazi katika maeneo ya utalii wamewekewa mipaka ya kutofika kwa baadhi ya Pwani kufanya biashara zao.

Olelei amefafanua kuwa wao hawana mgogoro na wananchi wala Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwani katika malezi ya jamii yao wamefunzwa kuheshimu jamii zingine na sheria kwa ujumla.
Posted by MROKI On Thursday, February 29, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo