Nafasi Ya Matangazo

December 21, 2023




Na Issa Mwadangala
Maafisa kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BOT) wamewataka Askari Polisi Mkoa wa Songwe kuwekeza kwa kufanya biashara ya kubadilisha fedha za kigeni kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza biashara hiyo.

Kauli hiyo imetolewa Disemba 20, 2023 na Mkuu wa Kitengo cha Uchunguzi Benki Kuu ya Tanzania (BOT) ndugu Amri Mbalilaki katika kikao na Maafisa, Wakaguzi na Askari wa vyeo mbalimbali wa Polisi Mkoa wa Songwe.

Ndugu Mbalilaki amesema kuwa, baada ya kufanyiwa mabadiliko ya sheria ya fedha za kigeni (SURA YA 271) zilizotengenezwa chini ya kifungu cha 5 (a) na 7 ya mwaka 2023 ambazo zinamtaka mtu zaidi ya mmoja kuanzisha biashara hiyo akiwa na milioni 200 tofauti na hapo awali mpaka uwe na Bilioni 01 ndio unaweza kuanzisha biashara hiyo.

“Hii sasa ni fursa kwa wadau mbalimbali mkiwemo Jeshi la Polisi kuweza kujitanua kimaisha katika njia tofauti tofauti kama hii ya kubadilisha fedha za kigeni kwa lengo la kufikia malengo katika maisha yetu ya kila siku.” alisema Mbalilaki.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi wa Polisi Theopista Mallya amewashukuru maafisa hao kwa elimu waliyoitoa na kuwataka Askari mkoani humo kuchangamkia fursa hiyo wakizingatia wapo mpakani na shughuli hizo hufanyika sana ili kuweza kufikia malengo waliojipangia katika maisha yao bila kuathiri utendaji kazi wa Jeshi la Polisi.

 Mkoa wa Songwe ni miongoni mwa mikoa ambayo inapakana na nchi jirani kama nchi ya Zambia na Malawi hivyo kufanya uwepo wa muingiliano mkubwa wa watu wa nchi hizo na Tanzania katika biashara.

Posted by MROKI On Thursday, December 21, 2023 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo