Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe.Rosemary Senyamule ametoa wito kwa wakandarasi wote waliopata nafasi ya kutekeleza miradi ya kimkakati katika jiji la Dodoma kuhakikisha wanakua na usimamizi mzuri kwa Watumishi wao kwa kufuata kanuni na taratibu za kiutumishi.
Wito huo umetolewa leo Novemba 8, 2023 wakati wa ziara ya kikazi ya ukaguzi wa miradi ya ujenzi wa barabara zilizo chini ya Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) pamoja na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) katika mradi wa barabara ya mzunguko wa nje (outer ringroad) ikiwa ni muendelezo wa ziara zake ambazo amekua akizifanya katika miradi inayoendelea kutekelezwa ndani ya Mkoa wa Dodoma.
"Niendelee kutoa wito kwa wote wanaopata nafasi za kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo, muhakikishe munafuata taratibu za utumishi ,tusingependa kuona masuala ya unyanyasaji kwa wafanyakazi hivyo hakikisheni mnatatua migogoro yote ili kuwezesha kukamilisha miradi kwa wakati " Ameeleza Mhe. Senyamule
Aidha, amewahimiza wakandarasi wakati wanapoendelea na utekelezaji wa Ujenzi wa barabara hiyo, kuhakikisha wanapanda miti yenye kuvutia pembezoni mwa barabara ili kupendezesha barabara, pia ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agenda ya kutunza Mazingira katika jiji la Dodoma.
Pia, Mhe. Senyamule amewasisitiza wakandarasi kukamilisha miradi kwa wakati na ubora unaotakiwa na ikiwezekana kuhakikisha wanakamilisha kabla ya muda uliopangwa wa miradi kukamilika .
Kwa Upande Wake, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Mhe.Jabir Shekimweri amewataka waajiri kuhakikisha wanajali maslahi ya Watumishi ili kuepusha changamoto za wizi wa vifaa vya kufanyia kazi .
Miradi ya Barabara iliyokaguliwa chini ya (TARURA) ni eneo la Mlimwa Ringi-Road yenye urefu wa Km 2.7 inayojengwa kwa kiwango cha Lami awamu ya tatu inayogharimu kiasi cha shilingi 2,577,534,902 ambapo hadi sasa umefikia asilimia 63, Barabara ya Bima yenye urefu wa Km 2.0 inayojengwa kwa kiwango cha Lami ngumu (asphalt concrete) inayogharimu kiasi cha 2,409,187,951.00 ambapo imefikia asilimia 33 hadi sasa na Barabara ya Mlimwa C (kuzunguka Makazi ya Waziri Mkuu) yenye urefu wa Km 2.6 inayogharimu kiasi cha 2,990,540,068.8 ambayo imefikia asilimia 72 kukamilika .
Awali alianza na barabara za Uwanja wa ndege wa Kimataifa Msalato na kumalizia barabara ya Mzunguko wa nje wa jiji la Dodoma yenye jumla ya urefu wa kilomita 112,3 kipande cha Veyula -Mtumba hadi Ihumwa yenye urefu wa kilomita 52.3 ambayo ilianza Septemba 20,2021 na inatarajiwa kukamilika Desemba 07,2024 na inagharimu kiasi cha shillingi 100,840,778,592.00 Ujenzi huo una lengo la kupunguza msongamano wa magari ndani ya jiji la Dodoma.
0 comments:
Post a Comment