Nafasi Ya Matangazo

October 30, 2023

Maonesho ya Sanaa Ziwani Nyanza yaliyohusisha michoro mbalimbali pamoja na uzinduzi wa sanamu ya mvuvi akiwa kwenye mtumbwi yamefanyika jijini Mwanza kwa lengo la kuelimisha jamii kutunza mazingira likiwemo Ziwa Victoria.

Maonesho hayo yamefanyika Jumamosi Oktoba 28, 2023 katika ufukwe wa Kamanga yakiandaliwa na shirika la mazingira na maendeleo EMEDO lililotoa mafunzo kwa wasanii wa michoro jijini Mwanza kwa kushirikiana na taasisi ya NAAM Festiva ya Kenya na Wasanii Visual Arts ya Dar es salaam kupitia mradi wa Sanaa Ziwani Nyanza unaofadhiliwa na ubalozi za Uswis na Noray nchini Tanzania.

Afisa mradi wa Sanaa Ziwani Nyanza kutoka shirika la EMDEO, Urthur Mjema amesema lengo la mradi huo ni kutumia sanaa ya michoro kuhamasisha jamii kuhusu utunzaji wa mazingira na hasa Ziwa Victoria kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

"Tusipotunza Ziwa hili halitakuwa na manufaa miaka ijayo kutokana na athari zinazoweza kusababisha vifo kwa viumbe hai ikiwemo samaki na dagaa. Tuna wajibu wa kuhakikisha hatutupi taka ovyo ikiwemo za plastiki" amesema Mjema.

Naye Afisa Uchechemuzi kutoka shirika la EMEDO, Mary Francis amesema shirika hilo limetoa mafunzo kwa wasanii wa michoro jijini Mwanza ili kuwajengea uwezo wa kutumia sanaa za michoro kuhamasisha jamii kutunza mazingira huku wakijipatia kipato.

"Moja ya kazi ya sanaa ni kutoa elimu, na hapa tunapeleka elimu kwa jamii ni jinsi gani taka zinaweza kuwa fursa kama zitatumika vizuri. Tunaona sanamu hii iliyotengenezwa kwa chupa za plastiki iliyookoa taka nyingi ambazo zingeingia ziwani na kuleta athari" amesema Afisa Utamaduni Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Agnes Majinge.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa wasanii wa michoro jijini Mwanza, Edward Tibasima amesema kupitia sanaa ya sanamu mvuvi iliyotengenezwa kwa chupa za plastiki, jamii itaelewa umuhimu kutumia taka kama mali ghafi badala ya kuzitupa ovyo na kuingia ziwani.

Mgeni rasmi kwenye maonesho hayo, Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Bhiku Kotecha ametoa rai kwa wananchi kuepuka uchafunzi wa mazingira hasa kutupa ovyo taka hususani taka za plastiki.

"Tunapokuwa kwenye vyombo vya usafiri kama daladala, mabasi na meli tuhakikishe tunatunza taka kwenye vyombo 'dustbin'. Si vyema unakunywa kinywaji na kutupa ovyo chupa, jiulize chupa za plastiki zilizotengeneza sanamu hii kama zingeingia ziwani hali ingekuwaje" ameshauri Kotecha.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Naibu Meya Jiji la Mwanza, Bhiku Kotecha akikata utepe kuashiria uzinduzi wa sanamu ya mvuvi akiwa kwenye mtumbwi iliyojengwa kwa taka za plastiki ili kuhamasisha matumizi ya taka hizo kama malighafi badala ya kuzitupa ovyo na kuathiri mazingira ikiwemo Ziwa Victoria.
Afisa Mradi wa Sanaa Ziwani Nyanza kutoka shirika la EMEDO, Arthur Mjema (kulia) akizungumza wakati wa maonesho ya michoro na uzinduzi wa sanamu ya mvuvi yaliyofanyika katika ufukwe wa Kamanga jijini Mwanza.
Afisa Uchechemuzi shirika la EMEDO, Mary Francis (kulia) akitoa ufafanuzi kuhusiana na mradi wa Sanaa Ziwani Nyanza unavyolenga kuhamasisha utunzaji wa mazingira kupitia sanaa za michoro.
Mkurugenzi wa taasisi ya NAAM Festival ya nchini Kenya, Dave Ojay (wa tatu kulia) akiwatambulisha wasanii wa michoro na vito jijini Mwanza waliopewa mafunzo na shirika la EMEDO ili kutumia sanaa yao kuelimisha jamii kuhusu utunzaji wa mazingira huku wakijipatia kipato.
Afisa Utamaduni Jiji la Mwanza, Agnes Majinge akizungumza wakati wa maonesho hayo. Kushoto ni Naibu Meya Jiji la Mwanza, Bhiku Kotecha.
Afisa Utamaduni Jiji la Mwanza, Agnes Majinge akizungumza kwenye maonesho hayo.
Mkurugenzi wa taasisi ya NAAM Festival ya nchini Kenya, Dave Ojay (kushoto) akitoa ufafanuzi wa michoro mbalimbali kwa Naibu Meya Jiji la Mwanza, Bhiku Kotecha (katikati). Kulia ni Afisa Jiji la Mwanza, Agnes Majinge.
Naibu Meya Jiji la Mwanza, Bhiku Kotecha akitazama michoro mbalimbali wakati wa maonesho hayo inayolenga kuelimisha jamii kuhusu utunzaji wa mazingira, Ziwa Victoria.
Naibu Meya Jiji la Mwanza, Bhiku Kotecha akitazama michoro mbalimbali wakati wa maonesho hayo inayolenga kuelimisha jamii kuhusu utunzaji wa mazingira, Ziwa Victoria.
Tazama hapa chini michoro mbalimbali iliyochorwa na wasanii waliopewa mafunzo na shirika la EMEDO kwa kushirikiana na taasisi ya NAAM Festiva na Wasanii Visual Arts ya Dar es salaam kupitia mradi wa Sanaa Ziwani Nyanza kwa ufadhili wa balozi za Uswis na Noray nchini Tanzania.

Tazama BMG TV hapa chini
Posted by MROKI On Monday, October 30, 2023 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo