Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa wameelekezwa kutoa elimu na maelekezo kwa wananchi wa Wilaya hiyo kuchukua tahadhari za kiusalama kuhusiana na tangazo la Mamlaka ya Utabiri wa hali ya hewa (TMA) kuhusiana na kuwepo uwezekanao wa kunyesha kwa mvua kubwa ya El-Nino ambayo inaweza kusababisha madhara hasa kwa wananchi wanaoishi maeneo hatarishi.
Maelekezo hayo kwa watumishi wote yametolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Bw. Ally Gugu Leo Oktoba 26, 2023 wakati akiendelea na ziara yake ya kikazi ya kufanya tathmini ya miradi na vyanzo vya mapato kwa Halmashauri, kukagua na kufuatilia miradi hiyo kwa kipindi cha Julai hadi Septemba katika Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Mkoa wa Dodoma.
"Ndugu zangu kama tunavyo endelea kuhimizwa na mamlaka ya hali ya hewa, tunatarajia kuwa na mvua nyingi mwaka huu (EL-NINO) kwa hiyo niendelee kusisitiza tuchukue tahadhari kwa kuweka mazingira wezeshi kwa kipindi hicho ili kujiepusha na athari zake " Amesisitiza Bw.Gugu
Bw.Gugu akiwa katika eneo la mradi wa Ujenzi wa ofisi ya Halmashauri ya Kongwa unaotekelezwa na Shirika la Uzalishaji Mali (JKT ) Kanda ya kati, ameonyesha kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa Jengo hilo na kusisitiza kutafuta mbinu mbadala ambayo itasadia kuongeza kasi ili uweze kukamilika kwa wakati kwa kuzingatia kiwango cha ubora ambapo hadi sasa mradi huo umefikia asilimia 41 ukiwa nyuma kwa siku 81.
"Fanyeni jitihada Kadri inavyo wezekana kulipa siku zilizo Chelewa kwa kuimarisha na kuongeza ufanisi ili kazi iweze kukamilika kwa wakati muafaka" Amesema Bw.Gugu
Hata hivyo ,wakati akikagua Shule ya Sekondari Mpya katika Kijiji cha Manungu kupitia fedha za mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) amewapongeza kwa kufikia asilimia 95 za utekelezaji wa Ujenzi wa mradi huo ambapo bado mambo madogo kuweza kukamilika.
Ujenzi huo unahusisha Vyumba vya madarasa 8, maabara 3, Maktaba 1, chumba cha TEHAMA 1, matundu ya vyoo 11, kichomea taka 1 na tanki la maji la ardhini 1.
Kwa Upande Wake, Mkurungezi wa Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Dr.Omary Nkullo amesema Halmashauri hiyo inaendelea kufanya majukumu yake kwa ufanisi unaotakiwa ili kutoangusha dhamira na jitihada za Serikali.
Bw.Gugu amefanikiwa
kutembelea miradi miwili ikiwemo ujenzi wa Ofisi ya Halmashauri ya Kongwa na Sekondari Mpya inayojengwa katika Kijiji cha Manungu.
Pia alipita kukagua nyumba ya kuishi ya Mkuu wa Wilaya ambayo inahitaji maboresho huku Mradi wa ujenzi wa nyumba ya Mkurungenzi Mtendaji ukiwa umekamilika.
0 comments:
Post a Comment