Rais wa Taasisi
ya Utafiti Tanzania ( ATARE) Prof
Joseph Ndunguru akiteta jambo na mwenyekiti wa taasisi hiyo Bw. Geoffrey Kirenga ambaye ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Kituo cha kuendeleza Kilimo nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania
(SAGCOT) kwenye mkutano na waandishi wa habari kuelezea malengo ya kuanzishwa kwa taasisi
hiyo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Rais wa Taasisi ya Utafiti Tanzania ( ATARE) Prof. Joseph Ndunguru (katikati )akifafanua jambo kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Jijini Dar es Salaam mwishoni wa wiki namna taasisi hiyo itakavyo watambua watafiti na tafiti wanazofanya ili zikatoe mchango stahiki katika kukuza uchumi wa Taifa. (Kushoto) ni mwenyekiti wa taasisi hiyo Bw. Geoffrey Kirenga ambaye ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Kituo cha kuendeleza Kilimo nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) na kulia ni Dkt. Elizabeth Maede********************
Na mwandishi wetu, Dar es Salaam
Taasisi ya Utafiti Tanzania (ATARE) imepania kuibua tafiti katika nyanja mbalimnbali ili kumsaidia mwananchi mmoja mmoja na kutoa mchango stahiki katika kukuza uchumi wa taifa.
Akieleza malengo ya ATARE kwa waandishi wa habari, Rais wa chama hicho, Prof. Joseph Ndunguru, alisema taasisi hiyo ilianzishwa ili kuwatambua watafiti na tafiti wanazofanya ili zisaidie kuleta tija endelevu katika kukuza maendeleo ya uchumi wa nchi na kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.
"Hiki ni chama kinachowakusanya pamoja watafiti wote Tanzania kutoka kada mbalimbal. Lengo ni kuhamasisha utafiti wa kisayansi na kiteknolojia kwa maendeleo endelevu. Aidha ni kuanzisha ushirikiano wa karibu utakaomsaidia wanachama kuendelea tafiti zake,”alisema Prof. Ndunguru.
Alieleza kuwa taasisi hiyo ina shabaha ya kuanzisha mfuko wa rasilimalifedha utakaosaidia kuendeleza tafiti mbalimbali na kuwajengea uwezo watafiti chipukizi ili nao waweze kuendeleza tafiti na kutoa michango stahiki katika kukuza uchumi wa taifa.
Aidha alisema pia umoja huo unataka kuwa jukwa la wanachama, kuanzisha mashirikiano ya kikazi na kuwawezesha na kuwatambua watafiti wabobezi na kuwa na kanzidata ya watafiti wote na tafiti wanazofanya.
“Watafiti wanamchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi. Kwa hiyo moja ya mipango yetu ni kuanzisha kanzidata itakayowatambua watafiti wote, kujua walipo na tafiti wanazofanya. Hili litarahisisha upatikanaji wa taarifa wa tafiti zote zilizofanyika Tanzania,”alisema Prof. Ndunguru.
Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Bw Geoffrey Kirenga ambaye ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Kuendeleza Kilimo Nyanda za Kusini mwa Tanzania (Sagcot) alisema kuna kazi kubwa ya kufanya ili utafiti umnufaishe na kumkomboa mkulima mdogo kwa kuzalisha kwa tija.
Alisema sekta ya kilimo inahitaji takribani sekta zote kuanzia sayansi ya viumbe, sayansi ya huandisi, sayansi ya jamii, sayansi ya masingira, sayansi ya nisharti zote ili uzalishaji uwe wa tija na kumnufaisha mkulima.
“Kwa kutofanya sayansi na kutokutumia dhana bora za uvunaji, nusu ya viazi ambavyo mkulima anazalisha vinabaki chini ya udongo na hivyo kutomnufaisha mkulima kwani anatumia gharama kubwa kuandaa shamba na mwisho wake anapata mavuno hafifu.
“Kabla ya kutumia mbinu za utafiti mkulima alikuwa anazalisha chini ya tani 7 kwa hekta ila baada ya kupewa mbinu bora za uzalishaji mkulima anazalisha tani 50 kwa hekta,” alisema Bw. Kirenga.
Kwa hiyo, alisema, mkulima wa Tanzania akiwezeshwa kwa kujengewa uwezo na kupewa teknolojia za kisasa za uvunaji anaweza akashindana na mkulima yoyote duniani wa zao la viazi na Tanzania ikaingia kwenye ramani za uzalishaji wa zao hilo.
“Tunaona pale Njombe Kijiji cha Rusitu Bi. Mgaya anaweza kuvuna tani 50 yani magunia 200 kutoka katika hekita. Hii ina maana kuwa kama mkulima wa Tanzania akiwezeshwa anaweza akashindana na mkulima yoyote duniani katika uzalishaji wa zao la viazi,” alisema Bw. Kirenga.







0 comments:
Post a Comment