Nafasi Ya Matangazo

September 27, 2023

Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Muragili (kulia), akimkabidhi Mwenge wa Uhuru, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Thomas Apson baada ya kumaliza mbio zake za kukagua miradi katika wilaya hiyo, Septemba 25, 2023.

*************
Na Dotto Mwaibale, Ikungi
KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023, Abdalla Shaib Kaim ameridhishwa na utekelezaji wa miradi yote illyopitiwa na kukaguliwa na Mwenge huo wilayani Ikungi mkoani Singida na kueleza kuwa imekamilishwa kwa viwango vya ubora wa hali ya juu ambao umeendana na thamani ya fedha.

Kaim akizungumza na wananchi wa wilaya hiyo Septemba 26, 2023 ikiwa ni siku yake ya nne ya mbio za mwenge alisema miradi yote ipo vizuri na kuwa mapungufu madogo madogo yaliyopo aliomba yafanyiwe kazi haraka ili kuiboresha zaidi.

Kiongozi huyo aliipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi kwa kubuni chanzo kipya cha mapato ambacho ni stendi mpya ya mabasi iliyojengwa eneo la Unyahati kutokana na fedha za mapato ya ndani.

“Niwapongeze kwa ubunifu mkubwa mlioufanya kwa kuanzisha stendi hii ambayo itakuwa chanzo kikubwa cha mapato,” alisema Kaim.

Aidha, aliagiza uongozi wa halmashauri hiyo kujenga vizimba kwa ajili ya kuwekea taka pamoja na kupanda miti kuzunguka stendi hiyo ili iwe katika mandhari nzuri.

Kaim alisema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa ikileta fedha nyingi kwenye halmashauri kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali hivyo ni jukumu la watendaji kuhakikisha wanaisimamia ili iwe inajengwa kwa viwango vya ubora ambavyo vinaendana na thamani ya fedha.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Thomas Apson akitoa  taarifa ya miradi iliyotembelewa na kukaguliwa na Mwenge wa Uhuru alisema ni saba na ina thamani ya Sh.Bilioni 2.14 na program mbalimbali tano.

Alitaja baadhi ya miradi iliyotembelewa kuwa ni mradi wa maji uliopo Kijiji cha Matare Kata ya Unyahati ambao umegharamiwa na fedha za Benki ya Dunia kupitia programu ya pforR uliotengewa Sh.386,898,900 na mradi wa ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa na matundu sita ya vyoo uliopo Shule ya Msingi ya Matare katika Kijiji cha Matare Kata ya Unyahati.

Alitaja miradi mingine kuwa ni Kitalu cha miti uliopo Kijiji cha Mungaa Kata ya Mungaa ambao tangu kuanzishwa kwake jumla ya miche 965,000 imezalishwa na kuwa unatekelezwa na Shirika lisilo la Kiserikali la Anti-Desert- Environment Scheme (ADESE) kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzani (TFS) na unafadhiliwa na Shirika lisilo la Kiserikali la Trees for the Future lililopo mjini Singida.

Apson alitaja miradi mingine kuwa ni Kikundi cha kufyatua matofali Vijana Chapakazi Ikungi ambacho kilianzishwa Desemba 6, 2022 na kukopeshwa mkopo wa Sh.Milioni 25 na Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi na ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Ikungi.

Alitaja programu zilizotembelewa na Mwenge huo kuwa ni ya mapambano dhidi ya Malaria na mapambano dhidi ya dawa za kulevya, damu salama, mapambano ya VVU, masuala ya lishe, mapambano dhidi ya rushwa na Ukimwi na usafi wa mazingira. 

Apson alisema Mwenge huo umekimbizwa umbali wa kilometa 137.7.ukifanya shughuli za uwekaji wa jiwe la msingi, uzinduzi na kutembelea miradi hiyo saba na kuwa kauli mbiu ya mbio hizo za Mwenge wa Uhuru 2023 ni Tunza Mazingira, Okoa Vyanzo vya maji kwa Ustawi wa Viumbe Hai na Uchumi.

Mbunge wa Viti Maalumu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)_Nusrat Hanje alipongeza kazi kubwa inayofanywa na Rais Samia kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Kwa dhati kabisa ya moyo wangu niipongeze Serikali ya  Rais Dk. Samia kwa kutuwezesha sisi watu wa Mkoa wa Singida na nimpongeze kaka yangu Mbunge Miraji Mtaturu kwa kusimamia vizuri miradi inayoletwa na kuhakikisha inakamilika kwa thamani ya fedha zilizotolewa,” alisema Hanje.

Akitoa salamu Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Singida, Aysharose Mattembe naye aliungana na viongozi wenzake akiwepo Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ikungi, Mika Likapakapa kumshukuru Rais Samia kwa kazi kubwa anayoifanya na kutoa fedha nyingi za kutekeleza miradi ambapo aliwaomba wananchi ilipo miradi hiyo kutunza miundombinu yake.

Kesho Septemba 27 timu nzima ya wakimbiza Mwenge huo wakiongozwa na Kiongozi wao wa Kitaifa wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2023, Abdalla Shaib Kaim watatembea na kukagua miradi mbalimbali katika Halmashauri ya Itigi.

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Thomas Apson  akimkabidhi Risala ya Utii Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023, Abdalla Shaib Kaim ili akamkabidhi Rais Samia Suluhu Hassan.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Ikungi, Rashid Rashid akiwa ameushika mwenge huo kabla ya kuanza kukimbizwa wilayani humo.
Vijana wa Skauti Khalid Abdallah (kushoto) na Mafongwe Tenga wakimvika Skafu Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023 wakati wakimkarisha Iilaya ya Ikungi kuanza kukimbiza mwenge huo.
Vijana wa Skauti wakimvika Skafu Mkimbiza mbio za Mwenge wa Uhuru, Atupokigwe Elia kutoka Dodoma wakati wakimkarisha Iilaya ya Ikungi kuanza kukimbiza mwenge huo

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023, Abdalla Shaib Kaim, akipanda mche wa mparachichi katika viwanja vya Shule ya Msingi Matare ikiwa ni kuhifadhi mazingira. BOFYA HAPA KUONA PICHA ZAIDI.

Posted by MROKI On Wednesday, September 27, 2023 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo