Nafasi Ya Matangazo

July 18, 2023

Mmoja Wa Wakulima Wa Zao La Kitunguu Mugisha Maico (Kushoto) Ambaye Mkazi Wa Mkoa Wa Mbeya Aliyeamua Kujiajiri Kwa Ajira Ya Kilimo Cha Umwagiliaji Katika Mto Manonga, Mbuga Ya Wembele Kitongoji Cha Magogo Kata Ya Isakamaliwa Tarafa Ya Igunga, Mkoani Tabora Akifanya Mahojiano Na Mwandishi Wa Habari Abdallah Amiri  
*************
Na Lucas Raphael,Tabora 
Katika kuunga mkono juhudi ambazo zimekuwa zikifanywa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassani ya kupambana na tatizo la kuondoa Changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana hapa nchini.
 
Baadhi ya makundi ya vijana zaidi ya 2000 wenye umri kuanzia miaka 25 hadi 35 kutoka nchi ya Tanzania, Uganda, Kenya na Rwanda wameamua kujiajiri wenyewe kupitia kilimo cha umwagiliaji katika mto Manonga uliopo Mbuga ya Wembele kitongoji cha Magogo kijiji cha Isakamaliwa kata ya Isakamaliwa tarafa ya Igunga wilaya ya Igunga mkoani Tabora.
 
Wakizungumza na waandishi wa habari waliofika katika kitongoji cha Magogo na kupiga kambi kwa siku mbili baadhi ya vijana hao Maico Rubeni kutoka mkoa wa Singida, Msakuo Omari kutoka Dar es saalam, Mugisha Maico kutoka Mbeya, Athumani Unyango kutoka nchi ya Kenya, Rwenda Vyarunge kutoka Rwanda, na Aron Jenyile kutoka Uganda.
 
Kwa nyakati tofauti walisema wameamua kujiajiri wenyewe kwa kulima mazao ya biashara ikiwemo vitunguu, mahindi, matikiti na nyanya baada ya kuona serikali ya Mama Samia imeboresha kwa kiasi kikubwa swala zima la upatikanaji wa pembejeo za kilimo ikiwemo mbolea na madawa ya kuua wadudu wanaoshambulia mazao.
 
Aidha vijana hao walisema swala jingine ambalo liliwashawishi kwenda huko Isakamaliwa kulima kilimo cha umwagilia  ni baada ya kupata taarifa kuwa eneo hilo lina mto mkubwa unaotunza maji kwa muda mrefu sambamba na Mbuga hiyo ya wembele kuwa na ardhi nzuri yenye rutuba ya kutosha.
 
“Jamani waandishi wa habari tunawashukuru kwa kututembelea  huku Isakamaliwa Kitongoji cha Magogo kwani umefika wakati sasa vijana tuache kuilaumu Serikali kila siku kwani hata kilimo ni ajira ya kudumu katika maisha endapo utalima kwa malengo. Hivi mnajua kuwa sasa gunia moja la vitunguu huku shambani ni Tsh. 300,000/= alisema Mugisha, huku akishangiliwa na wenzake.
 
Aidha Mugisha alibainisha kuwa wamekuwa wakilima mara mbili kwa mwaka huku akiongeza kuwa licha ya wao kunufaika na kilimo hicho cha umwagiliaji lakini pia Serikali imekuwa ikipata mapato ya kutosha kwa  kuwa wao wamekuwa wakilipa ushuru kila gunia moja Tsh. 1,000/=
 
Kufuatia hali hiyo waliwataka vijana wenzao waende katika kijiji hicho ili wakajiunge nao kwa kuendeleza swala zima la kilimo na kuacha tabia za kukimbilia mjini ambazo zinasababisha kujiingiza kwenye makundi ya uhalifu na kupoteza  nguvu kazi ya Taifa.
 
Hata hivyo walimpongeza Afisa kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga Grace Nyamwanji kwa kazi kubwa ambayo amekuwa akiifanya katika kata zote 35 za wilaya ya Igunga kwa kutoa elimu kwa wakulima ambapo imesaidia kwa wakulima kuelewa kilimo cha kitaalamu hali ambayo imekuwa ikisaidia hata wao kupata mazao mengi.
 
Aidha vijana hao wamemuomba Rais Samia kuendelea  kuajiri maafisa ugani kwa wingi ili kusaidia wakulima waweze kupata wataalamu wa kutosha kutoa elimu katika maeneo yao ambapo itawasaidia wakulima kuachana na kilimo cha kizamani.
 
Mwenyekiti wa kitongoji cha Magogo, Mwigulu Salumu alisema amefurahishwa sana na vijana hao kujiajiri wenyewe kupitia kilimo  cha umwagiliaji imeleta hamasa kubwa kwani hivi sasa Idadi ya vijana imeongezeka kufikia vijana zaidi ya 2000, na kusema kuwa Kitongoji hicho kina uwezo wa kulisha wilaya nzima ya Igunga na mkoa mzima wa Tabora kwa zao la mahindi na vitunguu.
 
Kwa upande wake Afisa  kilimo wilaya ya Igunga Grace Nyamwanji alishauri wakulima wote wa wilaya ya Igunga kuendelea kuzingatia elimu inayotolewa na maafisa kilimo kwenye mashamba yao huku akisema popote wanapoona wamekwama wasiache kuwaita maafisa kilimo.
 
Huku akibainisha kuwa  lengo la Serikali ya awamu ya sita ni kuhakikisha kila kijana anajikwamua kiuchumi kwa kusogezewa huduma karibu ya pembejeo za kilimo kama ilivyo sasa.
 
Nae Mtendaji wa Kata ya Isakamaliwa Misambo Kanyerere alitoa wito kwa  wafugaji kuacha tabia ya kupeleka mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima na badala yake waheshimu sheria za nchi kwani hatamvumilia  mfugaji yoyote atakayebainika kuanzisha migogoro inayoleta uvunjifu wa amani.

Posted by MROKI On Tuesday, July 18, 2023 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo