Waziri wa Utamaduni, Sanaa na na Michezo Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana akimkaribisha rasmi Kocha wa Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu (Taifa Stars) Adel Amrouche (katikati) baada ya kumtambulisha rasmi leo Machi 7, 2023 katika hafla fupi iliyofanyika Mtumba jijini Dodoma. Kulia ni Naibu Waziri wa wizara hiyo Mhe.Hamis Mwinjuma.
**************
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imesema kuwa katika kuendeleza mchezo wa Soka nchini itamlipa mshahara mwalimu wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), Adel Amrouche ambaye ni raia wa Ubelgiji mwenye asili ya Algeria .
Akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa kumtambulisha Kocha huyo, Machi 07, 2023 Mtumba jijini Dodoma, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema Serikali inaamini Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limejiridhisha kuwa ni Kocha Bora atakayekuza soka la Tanzania.
" Ukitazama wasifu wa Kocha Adel utabaini uzoefu mkubwa alionao sio tuu katika kufundisha soka uwanjani, bali pia katika kuandaa Wataalamu wengine wa Soka, hivyo tumtumie vizuri ili asaidie timu yetu kufanya vizuri ndani na nje ya nchi"
Ameongeza kuwa, Serikali inaendelea kuangalia uwezekano wa kupata Wataalamu katika michezo mingine ambapo ameeleza kuwa Wizara inaendelea kuimarisha Wataalamu wa michezo kupitia Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya kilichoko wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza.
Kwa upande wake Kocha Amrouche ameahidi kuwanoa wachezaji vyema ili kuiweka juu zaidi Tanzania katika ulimwengu wa Soka,huku akisisitiza ushirikiano kutoka kwa wadau mbalimbali katika kufanikisha kazi yake.
0 comments:
Post a Comment