Nafasi Ya Matangazo

March 11, 2023

Mkuu wa mkoa wa Arusha, John Mongella amezitaka taasisi mbalimbali kuhakikisha kunakuwepo na uwiano sawa wa jinsia kati ya wanaume na wanawake ili kuwepo kwa usawa mahala pa kazi. Ameyasema hayo jijini Arusha wakati akizungumza na wadau mbalimbali wa Benki ya CRDB walipokutana katika chakula cha jioni  kusherehekea siku ya wanawake duniani, iliyofanyika jana jijini humo.

Mongella alisema, hakuna agenda ya maendeleo inayoweza kufikiwa bila kukabiliana na changamoto zinazowakabili wanawake na kuweza kupatiwa ufumbuzi kwani wanawake ni jeshi kubwa na wana mchango mkubwa sana katika jamii.

"Naipongeza sana benki ya CRDB kwa namna ambavyo imejitahidi kukumbatia usawa wa kijinsia na kuweza kuwajengea uwezo wa kuwezesha wafanyakazi wa kike kwani nameambiwa asilimia 47 ya wanawake ni wafanyakazi wa benki hii huku wanaume wakiwa ni asilimia 53 na juhudi zaidi zinaendelea za kuongeza idadi ya wanawake ni mfano mzuri wa kuigwa na taasisi zingine. "amesema Mongela.
Kwa upande wake Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa Benki ya CRDB, Bruce Mwile amesema, kumekuwepo na ongezeko  la asilimia 3 la idadi ya wanawake katika benki hiyo tofauti na miaka ya nyuma na kuweza kuleta dhana nzima ya usawa wa kijinsia mahala  pa kazi.
 
Alisema benki hiyo ina programu ya kuwajengea uwezo wanawake katika ngazi ya kati ambapo wanawake mia moja wanashiriki katika programu hiyo huku lengo kuu ni kufikia idadi ya zaidi ya wanawake mia mbili ili kuleta usawa wa kijinsia.

"Kupitia kitengo cha biashara benki imeweza kufikia wanawake wadogo na wa kati kwa kutoa kiasi cha shs 67.3 bilioni hadi desemba 2022 ambapo jumla ya wanawake 3,122 wameweza kufikiwa katika mikoa yote Tanzania."amesema Bruce.

Aidha amesema kuwa, benki hiyo imeendelea kusisitiza jitihada zake katika maswala ya kijinsia na kukumbatia usawa katika jamii kwa ujumla ili kuondokana na changamoto ya kupigania usawa mahala pa kazi penye uwiano.
Kwa upande mwingine watoa mada mbalimbali walipata fursa ya kuchangia na kutoa wito kwa Wanawake nchini kujiamini na kuangalia fursa mbalimbali zilizopo na kuweza kuzichangamkia kwakua wao wanamchango mkubwa sana katika jamii kwa kuinua pato la taifa.

”Mwanamke ana uwezo mkubwa sana wa kuleta mabadiliko  katika jamii endapo atatumia fursa zilizopo kujikwamua kiuchumi bila kujali  nafasi hiyo inamhusu yeye au lah. alisema mchangia mada, Faraja Nyalandu.

Aliongeza kuwa, katika nyakati hizi za sayansi na teknolojia kila mmoja wetu anapaswa kwenda na mabadiliko yaliyopo sambamba na kuwa wabunifu katika maswala mbalimbali na kuwa kinara wa kuweza kutoa ajira kwa wanawake wengine.

Kwa upande wake Mshauri wa maswala ya ukimwi katika hospitali ya Olturumeti, Dk Consolata Swea akizungumza katika jukwaa hilo aliwataka wazazi wote kwa pamoja kuhakikisha wanasimamia malezi ya watoto wao kwani kwa.sasa hivi maadili yameporomoka kwa kiwango  kikubwa sana.

Aidha aliwataka wazazi kuwa marafiki wa watoto wao ili waweze kuwa wawazi katika kuelezea yale yote wanayofanyia na ndugu kwani kadri unavyokuwa karibu na mtoto ndivyo wanakuwa wawazi katika kueleza changamoto mbalimbali zinazowakabili.

"Kila mmoja anajua ukatili wanaofanyiwa watoto wetu na wanaofanya hivyo ni ndugu wenyewe wa familia na nawaomba sana msiwaamini ndugu kamwe wanapofika na wakati mwingine kulala na watoto kwani hao hao ndio wanawageuka."amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha ICT kutoka benki ya CRDB, Mwanaisha Kejo alisema kuwa,wanawake wana uwezo mkubwa wa kuyasemea maswala mbalimbali sambamba na kuendesha mabenki hivyo wanatakiwa  kujiongeza zaidi  na kufika viwango  vya juu zaidi.

Benki ya CRDB imeendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha mwanamke haachwi nyuma, na kila mwaka imekuwa ikiunngana na wadau wengi Duniani katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani ambayo huadhimisha kila ifikapo machi 8 ya kila mwaka.




Posted by MROKI On Saturday, March 11, 2023 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo