Nafasi Ya Matangazo

March 10, 2023

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amewataka watumishi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma kujibu kwa wakati barua za masuala ya kiutumishi ili kuepuka malalamiko yasiyo ya lazima ambayo yamekuwa yakielekezwa katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Mhe. Kikwete ametoa maelekezo hayo jijini Dodoma wakati wa kikao kazi chake na watumishi wa idara hiyo kilicholenga kufahamu majukumu yanayotekelezwa na kuhimiza uwajibikaji.

Mhe. Kikwete amewasisitiza watumishi wa idara hiyo ya Utawala wa Utumishi wa Umma kutosita kujibu barua za wadau kwa wakati hata kama zina mapungufu, ili wahusika wafahamu mapungufu yaliyopo kwenye masuala yao ya kiutumishi ambayo yamewasilishwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa ajili ya kupata kibali au kutolewa maamuzi.

“Natambua kuna mapungufu ya masuala ya kiutumishi katika barua mnazolalamikiwa kutozijibu kwa wakati, lakini mnapaswa kuzijibu kwani msipofanya hivyo, mnatoa mwanya kwa wahusika kuilalamikia ofisi na hatimaye kuichafua taswira nzuri ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,” Mhe. Kiwete amefafanua.

Aidha, amewataka watumishi wa idara hiyo kuchakata  utoaji wa vibali vya uhamisho wa watumishi wa umma kwa kuzingatia takwimu zinazoainishwa na Mfumo wa Tathmini ya Hali na Mgawanyo wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma ili vibali vya uhamisho vinavyotolewa visiathiri utendaji kazi wa baadhi ya taasisi katika eneo la utoaji huduma bora kwa wananchi.

Kuhusiana na utendaji kazi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma kwa ujumla, Mhe. Kikwete amewapongeza watumishi wa idara hiyo kwa kutekeleza majukumu yao kikamilifu licha ya kuwa ni mengi na yenye changamoto nyingi.

Mhe. Kikwete ameongeza kuwa, watumishi wa idara hiyo wanatakiwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kutimiza azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutoa huduma bora kwa wananchi.
Posted by MROKI On Friday, March 10, 2023 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo