Mkurugenzi wa
Huduma za Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi,
Mhandisi Aron Kisaka akizungumza na Wadau wa Bandari ya Ziwa Viktoria (hawapo
pichani) wakati alipofungua kikao cha kwanza cha wadau hao, kilichofanyika
jijini Mwanza.
Meneja wa
Bandari za Ziwa Viktoria Ferdinand Nyathi akifafanua jambo kwa Wadau wa Bandari hizo (hawapo pichani) wakati
wa kikao cha kwanza kilichowakutanisha kujadili mikakati na changamoto za bandari,
kilichofanyika jijini Mwanza.
Mtendaji Mkuu wa huduma za Meli (MSCL) Eric Hamiss akifafanua jambo kwa Wadau wa Bandari za Ziwa Viktoria (hawapo pichani) wakati wa kikao cha kwanza kilichowakutanisha wadau hao kujadili changamoto na mikakati ya kuboresha miundombinu na utendaji, kilichofanyika jijini Mwanza.
Baadhi ya wadau wakimsikiliza Mkurugenzi wa Huduma za Uchukuzi, kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Aron Kisaka (hayupo pichani) wakati wa kikao cha kwanza kilichowakutanisha wadau hao kujadiliana changamoto na mikakati ya kuboresha miundombinu na utendaji, kilichofanyika jijini Mwanza.************
Serikali imewataka wadau wa
bandari kutumia vyema fursa za vikao vinavyofanyika mara moja kwa mwezi ili
kuja na suluhu na mikakati madhubuti ya kuboresha huduma za usafiri na
usafirishaji nchini katika Ziwa Viktoria.
Akizungumza katika kikao cha
kwanza cha wadau wa maboresho ya bandari jijini Mwanza, Mkurugenzi wa Huduma za
Uchukuzi Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Mhandisi Aron Kisaka,
amesema kukutana pamoja kutawawezesha wadau kuwasilisha taarifa za utendaji
zinazoeleza mipango, mikakati na changamoto na namna ya kukabiliana na
changamoto ili kuwa na uelewa wa pamoja.
“Napenda kuwashukuru kwa
kushiriki katika kikao hiki na niwatake kuhakikisha yale yote tunayozungumza hapa
tujiwekee na ukomo ili vikao vinavyofuata tujipime kama tunakwenda mbele au
changamoto hizo ziende kwa mamlaka nyingine kwa maamuzi’ amesema Mhandisi
Kisaka.
Mhandisi Kisaka amewataka
wadau muhimu kama Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Nchini (TPA), Kampuni ya Huduma
za Meli (MSCL) na Wamiliki wa Bandari zilizorasimishwa Mkoani Mwanza kutafuta
masoko kwa nchi Jirani zinazotumia bandari za Kanda ya Ziwa ili kupata mzigo
mwingi zaidi na kuinua pato la taasisi hizo na wananchi kwa ujumla.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu
wa MSCL, Eric Hamis ameipongeza Serikali kwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili
ya ukarabati na ujenzi wa meli lengo likiwa kuhakikisha kuna mazingira mazuri
ya usafiri na usafirishaji katika Ziwa Viktoria.
Naye Meneja wa Bandari ya
Mwanza Ferdinand Nyathi, amesema kupitia vikao hivi mipango mbalimbali ya wadau
itawasilishwa kwa wadau ili kuwa na uelewa wa pamoja ambao matokeo yake itakuwa
ni kuboresha miundombinu kwa utaratibu mzuri ambao tija yake itakuwa ni
kuongeza pato la mamlaka, Taifa na mwananchi mmoja mmoja.
Meneja ameeleza mipango ya
bandari ni kujenga gati maalum kwa bandari ya Mwanza, Kemondo na Kagera kwa
ajili ya kuhudumia meli kubwa zaidi ikiwemo ya MV Mwanza hapa kazi tu ambayo
inakamilishwa.
Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta
ya Uchukuzi) inaendelea na mpango wake wa kusimamia vikao vya wadau wa
maboresho ya bandari katika Bandari za Bahari ya Hindi, na kwenye Maziwa nchini
lengo ni kuhakikisha bandari zinaleta ufanisi na tija na hatimaye kurahisisha
shughuli za usafiri na usafirishaji nchini.
Imetolewa na Kitengo cha
Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.
0 comments:
Post a Comment