Nafasi Ya Matangazo

December 29, 2022

Edson Arantes do Nascimento au maarufu Pele amefariki duania akiwa na umri wa miaka 82. 

Mchambuzi wa habari, rafiki yangu Maggid Mjengwa anaandika machache kuhusu kiumbe huyu gwiji wa kupachika mabao awapo uwanjani akilisakata gozinla Ng'ombe.

Anasema Pele, itakumbukwa, kuwa   ulimwengu wa kandanda ulishuhudia ujio wa mchezaji aliyekuwa na umri mdogo kuliko wengine wote katika fainali za Kombe la Dunia kwa mwaka 1958 kule nchini Sweden. Kijana huyu mdogo alikuwa na miaka 17 tu, aliitwa Pele.

Ni mchezaji huyu mdogo ambaye nyota yake iliyoanza kung'aa akiwa Sweden, ikaja kung'aa zaidi na kuacha simulizi zitakazodumu milele. Mchango wake ukaja pia kuibadili  soka ya dunia. 

Binadamu mwenzetu huyu ambaye ni maarufu kwa jina moja la Pele ana jina lake kamili ambalo ni refu kidogo. Anaitwa Edson Arantes do Nascimento.

Pele alizaliwa Oktoba 23 mwaka 1940. Kitu pekee kilichompambanua Pele kutoka kwa wachezaji wengine ni uwezo wake mkubwa wa kufunga mabao.

Kulingana na taarifa rasmi, inaaminika, kuwa Pele amefunga magoli 1281 kati ya mechi 1363 alizopata kucheza. Huo ni wastani wa goli 0.9398 kwa kila mechi! Kwa hesabu hizo za kitaalam, hakuna mchezaji mwingine yeyote duniani aliyepata kukaribia rekodi hiyo.

Akiwa na timu ya taifa ya Brazil, Pele alipata kufunga magoli 77 kati ya mechi 92 alizocheza. Hiyo ni rekodi kwa taifa la Brazil, lakini si rekodi ya dunia. Rekodi ya dunia hadi sasa inashikiliwa na mchezaji Ali Daei wa Iran aliyepata kufunga magoli 104 akiwa na timu ya taifa ya nchi yake.

Labda tukio lililosubiriwa na wapenzi wengi wa kandanda ni lile la mchezaji huyo nyota  kufunga goli lake la 1000. Goli hilo lilifungwa na Pele katika mechi yake ya 909 mnamo mwaka 1969.
Alilifunga kwa penalti  akiwa na klabu yake ya Santos.

Mwaka 1959 utakumbukwa kama mwaka ambao Pele alipachika nyavuni  magoli mengi zaidi kuliko miaka mingine yote akiwa mchezaji.
Katika mechi zote za mwaka huo, Pele alipachika  jumla ya magoli 126.

Pele hakuwa tu sumu kali katika kufunga magoli, Pele aliogopewa na timu pinzani pia. Alikuwa hodari karibu kwa kila kitu alipokuwa uwanjani. Alikuwa na ufundi mkubwa. 

Pele alikuwa na  uelewa mkubwa wa mchezo. Aliweza kupiga mashuti makali kwa miguu yote miwili na alikuwa hodari kwa kupiga mipira ya adhabu ndogo. 

Pele huyu alikuwa hodari pia kwa kutoa pasi "zenye macho". Pasi zake zilikuwa za uhakika kana kwamba alifunga pimamaji miguuni. 

Ingawa Pele hakuwa mrefu sana, lakini alikuwa na uwezo mkubwa wa kucheza mipira ya juu. Aliweza kuruka na kuipata mipira mingi ya vichwa.
 

Posted by MROKI On Thursday, December 29, 2022 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo