Na Mwandishi wetu, Dar
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya watu wa China zimeahidi kuendeleza ushirikiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizo kwa kuzingatia misingi ya ushirikiano wa kirafiki kwa maslahi mapana ya mataifa yote mawili.
Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) alipokutana kwa mazungumzo na Balozi wa China nchini, Mhe. Chen Mingjian katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Waziri Mulamula amesema katika mazungumzo yao wamejadili masuala mbalimbali, ikiwemo suala la namna ya kuimarisha misingi ya ushirikiano baina ya mataifa hayo.
"Tanzania tutaendelea kuzingatia kwa dhati kanuni ya kuwa na China moja, kuunga mkono kwa dhati msimamo halali wa China, kuunga mkono China katika kulinda maslahi yake ya msingi," amesema Waziri Mulamula
Kwa Upande wake Balozi wa China nchini, Mhe. Mingjian amesema kuwa Serikali yake wakati wote imekuwa rafiki mzuri kwa Serikali ya Tanzania na kwamba urafiki wa nchi hizo mbili umekuwa mfano mzuri wa kuigwa na China itaendelea kuheshimu na kuenzi urafiki huo.
"Tunathamini ushirikiano kati ya Tanzania na China, uhusiano huu umejengwa katika misingi imara na isiyotikisika…..China itaendelea kusisitiza dhamira yake ya kuimarisha uhusiano bora kati yake na Tanzania," amesema Balozi Mingjian.
Uhusiano kati ya Tanzania na China ulianza mapema miaka ya 1960 wakati nchi hizo mbili zilipoanzisha uhusiano wa kidiplomasia tarehe 9 Desemba 1961.
0 comments:
Post a Comment