Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiongoza kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika leo tarehe 21/01/2019 Ikulu jijini Dar es Salaam.
Baraza la Mawaziri limeridhia utozwaji wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa kiwango cha asilimia sifuri kwenye umeme unaouzwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO) na kufuta malimbikizo ya deni la kodi ya VAT lililofikia shilingi Bilioni 22.9 kwa TANESCO kwenye umeme uliouzwa ZECO.
Baraza la Mawaziri limeridhia utozwaji wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa kiwango cha asilimia sifuri kwenye umeme unaouzwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO) na kufuta malimbikizo ya deni la kodi ya VAT lililofikia shilingi Bilioni 22.9 kwa TANESCO kwenye umeme uliouzwa ZECO.
Baraza
la Mawaziri limefanya uamuzi huo leo tarehe 21 Januari, 2019 Ikulu Jijini Dar
es Salaam, katika kikao kilichoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe.
Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.
Dkt. Ali Mohamed Shein, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi na
Mawaziri.
Akizungumza
baada ya kikao hicho Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Magufuli amesema baada ya kufanya uamuzi huo
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango atawasilisha marekebisho madogo
ya sheria ya VAT, sura ya 148 kupitia sheria ya fedha ya mwaka 2019 ili umeme
unaouzwa Tanzania Zanzibar utozwe VAT kwa kiwango cha asilimia sifuri.
“Kwa hiyo
madeni yatakayokuwa yanadaiwa kwa Zanzibar ni yale madeni ya kulipia umeme,
umeme wametumia kiasi fulani wanalipa kama wanavyolipa wa maeneo mengine kwa
mfano wanavyolipa Dar es Salaam, suala la kutoza VAT sasa halipo, na katika
hilo kwa sababu kulikuwa na deni ambalo lilikuwa limefika shilingi Bilioni
22.9, sisi Baraza la Mawaziri tutapeleka mapendekezo Bungeni kwamba lisamehewe
kwa sababu lipo ndani ya bajeti ya mwaka huu wa 2018/19, kwa hivyo litapunguza
mapato yatakayotakiwa kukusanywa na Serikali”
amesema Mhe. Rais Magufuli.
Kwa
upande wake Mhe. Dkt. Shein amesema pamoja kuridhia utozaji wa VAT kwa kiwango
cha asilimia sifuri, Baraza la Mawaziri pia limekubaliana kuwa Makamu wa Rais,
Mhe. Samia Suluhu Hassan ataitisha vikao vya kuzungumzia masuala ya Muungano
kila mara kunapokuwa na hoja ya masuala ya Muungano ili kujadili na kutoa
uamuzi.
“Tungependa
sana mambo haya yafanyike vizuri kwa sababu pande mbili za Muungano zinatuhusu
sote, hili ni muhimu kwa sababu mambo yakikusanyika mengi wananchi wanahisi
hatusaidii jitihada zao, kwa hivyo tumeridhia kuwa masuala ya Muungano ambayo
yapo chini ya Makamu wa Rais, wakae pamoja wayajadili ili yapate uamuzi wa
pande zote mbili” amesema Mhe. Dkt. Shein.
Wakati huo huo,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
amemuapisha Mhe. Anjellah Jasmine Mbelwa Kairuki kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu Uwekezaji.
Mhe.
Kairuki ameapishwa kabla ya kuanza kwa kikao cha Baraza la Mawaziri, kufuatia
mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Mhe. Rais Magufuli
tarehe 08 Januari, 2019 ambapo Mhe. Kairuki aliyekuwa Waziri wa Madini
aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji.
0 comments:
Post a Comment