Nafasi Ya Matangazo

July 11, 2026

 



Dar es Salaam
Mjiolojia kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Njombe, Abbas Mruma, amesema Tanzania inaendelea kujijengea nafasi muhimu duniani kutokana na kuwa na hifadhi kubwa ya madini muhimu ya kimkakati, yakiwemo graphite, lithium na rare earth elements, ambayo ni nguzo muhimu katika maendeleo ya teknolojia za kisasa na nishati safi.

Mruma ameyasema hayo wakati akitoa maelezo kwa Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Richard Stanslaus Muyungi, alipotembelea banda la Tume ya Madini katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba).

Amesema mahitaji ya madini ya lithium yanaendelea kuongezeka kwa kasi duniani kutokana na matumizi yake katika utengenezaji wa betri za magari ya umeme, simu za mkononi, kompyuta mpakato (laptops) na vifaa vingine vya kisasa vya kielektroniki.

Amefafanua kuwa nchini Tanzania, madini ya lithium yanapatikana zaidi katika maeneo ya Dodoma na Ikungi, mkoani Singida.

Akizungumzia madini ya graphite, Mruma amesema Tanzania ndiyo nchi inayoongoza barani Afrika kwa kuwa na hifadhi kubwa ya madini hayo, ambayo ni malighafi muhimu katika utengenezaji wa betri za magari ya umeme pamoja na matumizi mengine mbalimbali ya viwandani.

Aidha, amesema Tanzania pia ina hifadhi kubwa ya madini ya rare earth elements katika Ukanda wa Afrika Mashariki, yanayopatikana katika eneo la Ngualla mkoani Songwe na Wigu mkoani Morogoro.

Baada ya kupokea maelezo hayo, Dkt. Richard Stanslaus Muyungi ameipongeza Tume ya Madini kwa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu rasilimali za madini na fursa zilizopo katika sekta hiyo.

Amesema elimu hiyo ina mchango mkubwa katika kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa rasilimali za madini, fursa za uwekezaji na nafasi ya sekta ya madini katika kukuza uchumi na maendeleo endelevu ya Taifa.
Posted by MROKI On Saturday, July 11, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo