Nafasi Ya Matangazo

August 10, 2018

 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza na wananchi wa kijiji cha Likunja Wilayani Ruangwa, akiwa kwenye ziara yake ya kikazi ya siku nne, Agosti 10.2018 (Picha na Ofisi ya Naziri Mkuu)
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza na wananchi wa kijiji cha Likunja Wilayani Ruangwa, akiwa kwenye ziara yake ya kikazi ya siku nne, Agosti 10.2018 
 Wananchi wa kijiji cha Likunja wakimsikiliza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, aliposimama na kuzungumza nao, akiwa kwenye ziara yake ya kikazi ya siku nne Wilayani Ruangwa, Agosti 10.2018
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imetenga sh. bilioni tano katika mwaka wa fedha wa 2018/2019 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara ya Nanganga-Ruangwa yenye urefu wa kilomita 57 kwa kiwango cha lami.

Ameyasema hayo leo (Ijumaa, Agosti 10, 2018) wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Likunja wilayani Ruangwa akiwa katika siku ya tatu ya ziara yake ya kikazi wilayani hapa.

Waziri Mkuu amesemaSerikali imeendelea kuboresha huduma za jamii nchini kwa kujenga miundombinu mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara ili kurahisisha usafiri wa watu na mizigo.

Amesema ujenzi wa barabara hiyo ya Nanganga-Ruangwa-Nachingwea hadi Masasi unatarajiwa kuanza hivi karibu, hivyo amewataka wananchi waendelee kuwa na imani na Serikali yao.

Akizungumza kuhusu nyumba zilizowekewa alama ya X, Waziri Mkuu aliwataka wahusika wazibomoe wenyewe ili kupisha ujenzi wa barabara hiyo kwa kuwa walivamia eneo na watakaosubiri hadi Serikali iwabomelee watalazimika kuilipia gharama, hivyo ni vema wakatii.

Wakati Huo huo,Waziri Mkuu amesema Serikali imedhamiria kumaliza tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika maeneo mbalimbali nchini, ambapo asilimia 95 ya vijiji vyote vya wilaya ya Ruangwa vinapata huduma hiyo.

Waziri Mkuu ameyasema hayo baada ya wananchi wa kata hiyo kueleza changamoto zinazowakabili ikiwemo huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama.

“Tumeendelea kuboresha huduma za jamii katika vijiji vyote vikiwemo na vya wilaya hii. mkakati wetu ni kuhakikisha wananchi wote mnapata maji katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yenu na tayari asilimia 95 ya vijiji vinapata maji,” amesema.

Kuhusu changamoto ya zahanati ya  kijiji cha Likunja kutokuwa na nyumba ya mganga, Waziri Mkuu amewashauri wananchi hao wafyatue matofali na kisha waanze ujenzi wa boma na Halmashauri itawasidia kuwapa vifaa vya viwandani kama saruji, mabati na misumari.
Posted by MROKI On Friday, August 10, 2018 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo