Mwandishi Wetu
WAGONJWA wengi wenye tatizo la shinikizo la damu hushindwa kufanya mazoezi ya mwili
kutokana na ukweli kwamba, yanalazimisha moyo kufanya kazi ya ziada.
Wagonjwa
wengi wa moyo wanapojaribu kufanya mazoezi, hukabiliwa na uchovu pamoja na
kushindwa kuongeza pumzi.
Dalili hizi
huwafanya wengi wao kuishi bila kuushughulisha mwili, jambo ambalo huathiri
zaidi afya zao, mipango yao ya kiuchumi na ubora wa maisha kwa ujumla.
Ingawa mazoezi
hufikiriwa kuwa ni hatari kwa wagonjwa wenye maradhi ya moyo, tafiti za hivi
karibuni zinabainisha kuwa mazoezi ni muhimu sana kwa watu wenye maradhi haya.
Tafiti za
kitabibu zinaonesha kuwa, mazoezi huwasaidia wagonjwa wa moyo kutumia hewa ya
oksijeni vizuri na kwa faida.
Mazoezi pia
huongeza mzunguko wa damu katika misuli mwilini na hupunguza kiasi cha lehemu
mbaya mwilini, uwezekano wa kupata magonjwa yatokanayo na uvimbejoto, uwezekano
wa kulazwa hospitalini mara kwa mara, matumizi ya dawa na vifo vya mapema.
Hii ni kwa
mujibu wa Julie Adsett na Robbie Mullins wa Chuo Kikuu cha Teknolojia cha
Queensland cha Uingereza, katika chapisho lao la ushahidi wa kisayansi kuhusu
faida za mazoezi kwa watu wenye maradhi ya moyo ya muda mrefu, lililotolewa mwaka
2010.
Katika
makala yake iliyochapishwa katika jarida la Chama cha Madaktari wa Marekani (JAMA)
toleo la 288(16) la mwaka 2002, Dk. Jonathan Myers (PhD) wa kitengo cha
magonjwa ya moyo katika Chuo Kikuu cha Stanford nchini Marekani, anasema kwamba
wagonjwa wapya wanaogunduliwa kuwa na shinikizo la damu, wanapata nafuu haraka
wanaposhiriki katika mazoezi. BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI MAKALA HAYA.
Lakini
wanaweka bayana kuwa kabla ya kuanza programu ya mazoezi, watu wenye maradhi ya
moyo wanahitaji kupata uchunguzi na uangalizi wa karibu wa daktari bingwa.
Wagonjwa hawa wanashauriwa kufanya mazoezi mepesi na wasitumie muda mrefu sana.
Watu wenye
matatizo ya moyo wanaweza kufanya mazoezi ya kutembea, kukimbia taratibu na
kuendesha baiskeli kwa mwendo mdogo. Watu hawa pia wanaweza kufanya mazoezi ya
kunyoosha misuli pamoja na kukunja na kukunjua viungo vya mwili mara kwa mara.
Mambo ya kuzingatia
Inashauriwa
kuepuka mazoezi yanayohusisha kubeba uzito mkubwa na mazoezi kama vile pushapu.
Pia ni vizuri kujiepusha na mazoezi katika sehemu zenye baridi kali hasa nje ya
nyumba au katika sehemu zenye joto kali sana.
Wataalamu
wa tiba za mazoezi wanapendekeza kuanza kwa mazoezi mepesi na taratibu, huku
ukiongeza kadri siku zinavyokwenda na kwa kadri unavyoendelea kujisikia vizuri.
Simamisha mazoezi mara moja pale unapojisikia kuchoka, kizunguzungu, moyo
kudunda bila mpangilio, kifua kuuma, kichefuchefu au kuishiwa pumzi.
Andika
kwenye daftari dalili yoyote inayojitokeza, wakati ilipotokea na aina ya
mazoezi uliyokuwa unafanya wakati dalili hiyo ilipojitokeza. Mweleze daktari
wako kuhusu taarifa hizo pale utakapokwenda kupata ushauri au huduma za
kitabibu. Usifanye mazoezi kama hujisikii vizuri au kama ulikuwa mgonjwa sana
katika siku za karibuni.
Kabla ya
kufanya mazoezi pima mapigo yako ya moyo na kama yako zaidi ya 100 kwa dakika
katika hali ya kupumzika, usifanye mazoezi na badala yake nenda kamuone daktari
kwa ushauri wa kitabibu.
Kama mapigo
ya moyo yatakuwa sawa kabla ya mazoezi, unatakiwa kupima tena baada ya mazoezi
mepesi na kuona kuwa mapigo ya moyo yanarudi katika hali ya kawaida ndani ya
dakika kumi baada ya kusimamisha mazoezi.
Usifanye
mazoezi muda mfupi baada ya kula. Subiri angalau zipite dakika 90 ndipo ufanye
mazoezi. Ili kupata faida zaidi, fanya mazoezi unayoyapenda, yanayokufurahisha
na yasiyo kupotezea mapato yako.
Mazoezi ni
nini?
Mzoezi
siyoi lazima kwenda kwenye vituo maalumu vya mazoezi. Wataalamu wa afya
wanaeleza kuwa jambo lolote ambalo mtu atafanya kwa kuushughulisha mwili wake
kwa kusababisha viungo vifanye kazi na hata kumsababishia atoke jasho
linatafsiriwa kuwa ni sehemu ya mazoezi.
Kwa sababu
hiyo wanayataja baadhi ya mambo ambayo yanaweza kuwa sehemu ya mazoezi kuwa ni
kazi za kutoa jasho, kutembea, kukimbia kukimbia, michezo au mazoezi kulingana
na wataalamu.
Baadhi ya
mambo ambayo watu wanafanya na ikawa ni sehemu ya mazoezi ni kama vile
kuendesha baskeli, kutembea, kulima pamoja na kazi nyingine zinazotoa jasho.
Hata hivyo,
wataalamu wa afya wanashauri wenye matatizo ya moyo wanapaswa kufanya mazoezi
kwa maelekezo na usimamizi wa mtaalamu wa afya mwenye taaluma kuhusu magonjwa
ya moyo.
Makala haya yameandaliwa na Chama cha
Waandishi wa Habari Wanaopambana na Magonjwa Yasiyo ya Kuamukiza (TJNCDF) kwa
kushirikiana na Chama cha Ugonjwa wa Kisukari Tanzania (TDA). Maoni au maswali
tuma TJNCDF, S.L.P 13695, Dar es Salaam.
0 comments:
Post a Comment