Nafasi Ya Matangazo

October 30, 2017

MBUNGE wa Jimbo la Singida Kaskazini, kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Lazaro Nyalandu ametangaza kujiuzu nafasi zake zote za uongozi ndani ya CCM.

Aidha Nyalandu amemuandikia barua Spika wa Bunge wa Job Ndugai kumweleza adhma yake ya kujivua nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Singida Kaskazini.

Taarifa iliyotolewa na Mbunge huyo kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii na kunukuliwa na FATHER KIDEVU BLOG  hii imeeleza sababu mbalimbali za kujiuzulu kwake nyadhifa hizo.

TAARIFA HIYO INASOMEKA HIVI:- 
“NIMEAMUA kujiuzulu NAFASI yangu ya Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi CCM, pamoja na nafasi zote za Uongozi ndani ya Chama kuanzia leo, Oktoba 30, 2017.

HALIKADHALIKA, asubuhi ya leo nimemwandikia Spika wa Bunge, Mh. Job Ndugai, Mb., barua ya kujiuzulu nafasi yangu ya UBUNGE wa Jimbo la Singida Kaskazini kupitia tiketi ya CCM, nafasi ambayo nimeitumikia kwa vipindi vinne mfululizo tangu nilipochaguliwa kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 2000 hadi Sasa.

AIDHA, Nimechukua UAMZI huo kutokana na kutorishwa kwangu na mwenendo wa hali ya Kisiasa nchini, ikiwa ni pamoja na ukiukwaji wa HAKI za Kibinadamu, ongezeko la vitendo vya dhuluma wanavyofanyiwa baadhi ya watanzania wenzetu, na kutokuwepo kwa mipaka ya wazi kati ya MIHIMILI ya dola (Serikali, Bunge, na Mahakama) kunakofanya utendaji kazi wa Kibunge wa Kutunga Sheria na wa Kuisimamia Serikali kutokuwa na uhuru uliainishwa na kuwekwa bayana KIKATIBA.


VILEVILE, Naamini kwamba bila Tanzania kupata Katiba Mpya Sasa, hakuna namna yeyote ya kuifanya mihimili ya dola isiingiliane na kuwepo kwa ukomo wa wazi na kujitegemea kwa dhahiri kwa mihimili ya Serikali, Bunge na mahakama ambayo ndio chimbuko la Uongozi Bora wa nchi, na kuonesha kwa uwazi kuwa madaraka yote yatokana na wananchi wenyewe, na kwamba Serikali ni ya Watu kwajili ya Watu.


Mimi Naondoka na kukiacha Chama Cha Mapinduzi CCM, nikiwa nimekitumikia kuanzia ngazi ya Uenyekiti wa UVCCM Mkoa, Ujumbe wa Kamati za Siasa Wilaya na Mkoa, Ujumbe wa Kamati ya Wabunge Wote wa CCM na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM TAIFA, kwani nimejiridhisha kuwa kwa mwenendo wa hali ya kisiasa, kiuongozi na kiuchumi uliyopo Tanzania Sasa, CCM imepoteza mwelekeo wake wa kuisimamia Serikali kama ilivyokuwa hapo awali.

AIDHA, Naamini kuwa, kama ilivyotokea kwa mihimili ya Bunge na Mahakama kutokuwa na uhuru kamili, bila kuingiliwa kiutendaji kwa namna Moja au nyigine, CCM nayo imekuwa Chini ya miguu ya dola badala ya chama kushika hatamu na kuikosoa Serikali inapobidi kama yalivyokuwa maono ya Baba wa TAIFA MWALIMU Julius Kambarage Nyerere”, Mwisho wa nukuu.


Posted by MROKI On Monday, October 30, 2017 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo