Nafasi Ya Matangazo

August 11, 2016

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akihutubia maelfu ya wananchi wa mkoa wa Mwanza na maeneo ya kanda ya ziwa katika mkutano wa hadhara katika uwanja wa Furahisha eneo la Kirumba jijini humo

Wananchi wa Mwanza wakimsikiliza Rais Magufuli.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameviagiza vyombo vya dola kuchunguza na kuchukua hatua za kurejesha mali za Chama Kikuu cha Ushirika cha Ushirika cha Nyanza ambazo zilinunuliwa na kutwaliwa na watu binafsi kwa njia za ujanja ujanja.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 11 Agosti, 2016 alipokuwa akiwahutubia wananchi wa Mwanza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Furahisha Jijini Mwanza.

Dkt. Magufuli amesema Serikali yake haipo tayari kuwafumbia macho watu wachache waliovifilisi vyama vya ushirika vya wakulima kwa kujimilikisha mali za ushirika yakiwemo majengo, viwanda na mashamba na ametaka mali hizo zirudishwe mikononi mwa wananchi.

"Hata kama walichukua miaka 20 iliyopita, vyombo vya dola vichukue hatua na mali hizo zirudishwe kwa umma" Amesema Rais Magufuli.

Katika Mkutano huo Rais Magufuli pia amesema Serikali itafanya oparesheni kubwa ya kuteketeza Makokoro katika ziwa Victoria ikiwa ni juhudi za kukabiliana na tatizo la uvuvi haramu uliosababisha kupungua kwa samaki na kuathiri shughuli za uvuvi na usindikaji wa minofu ya samaki katika viwanda.

Amebainisha kuwa lengo la kuchukua hatua hiyo ni kuwezesha samaki wengi kuzaliana ili lengo la Serikali la kujenga viwanda vya kusindika mazao ikiwemo viwanda vya kusindika minofu ya samaki lifanikiwe.

Kabla ya kuhutubia mkutano huo Rais Magufuli ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja la waenda kwa miguu la Furahisha linalokatiza barabara ya Uwanja wa Ndege kwenda katikati ya Jiji la Mwanza.

Daraja hilo litakuwa na urefu wa meta 46, upana wa meta 3.6 na kimo cha meta 5.5 na ujenzi wake unatarajiwa kukamilika Mwezi Desemba Mwaka huu kwa gharama ya Shilingi Bilioni 6.455

Akizungumzia ujenzi huo Rais Magufuli amemtaka Mkandalasi anayejenga Daraja la Furahisha kukamilisha kazi hiyo Mwezi Desemba Mwaka huu kwa mujibu wa mkataba, na pia ameagiza Mkandalasi aliyekuwa akifanya upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza kuendelea na kazi hiyo ndani ya wiki moja kwa kuwa Serikali imejipanga kumlipa fedha za kazi hiyo.

Pia Dkt. Magufuli ameahidi kuongeza fedha katika ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Katikati ya Jiji la Mwanza hadi Uwanja wa Ndege wa Mwanza ili barabara hiyo ifike hadi uwanjani badala ya kuishia eneo la Pasiansi.
Posted by MROKI On Thursday, August 11, 2016 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo