Nafasi Ya Matangazo

July 04, 2016




 Moja ya mabasi hayo yalimulikwa tochi hii leo yakiwa spidi 122.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa familia za watu 29 waliopoteza maisha katika ajali ya barabarani iliyosababishwa na mabasi mawili ya kampuni moja ya City Boy kugongana uso kwa uso katika kijiji cha Maweni, kilichopo katika tarafa ya Kintinku, Wilaya ya Manyoni Mkoani Singida.

Ajali hiyo imetokea leo tarehe 04 Julai, 2016 majira ya saa tisa alasiri wakati basi moja la kampuni ya City Boy lenye namba T531DCE lililokuwa likisafiri kutoka Jijini Dar es salaam kwenda Kahama Mkoani Shinyanga lilipokuwa likipishana na basi jingine la kampuni hiyo hiyo ya City Boy lenye namba T247DCD lililokuwa likisafiri kutoka Kahama Mkoani Shinyanga kwenda Jijini Dar es salaam.

Rais Magufuli ametuma salamu zake kwa familia zilizopatwa na msiba huo kupitia kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi Methew Mtigumwe na kuelezea masikitizo yake juu ya kutokea kwa ajali hiyo mbaya, iliyosababisha watu wengi kufariki dunia.

"Nimepokea kwa mshituko mkubwa taarifa za ajali hii ambayo imesababisha vifo vya idadi kubwa ya watanzania, kwa hakika nimesikitishwa sana sana na napenda kuungana na familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.

"Namuomba Mwenyezi Mungu awape uvumilivu na ustahimilivu wanafamilia wote waliopoteza jamaa zao, na sote tuwaombee marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi, amina." Ameeleza Rais Magufuli.

Aidha, Dkt. Magufuli amewaombea majeruhi wote wa ajali hiyo, ambao wanapatiwa matibabu hospitali wapate nafuu na kisha kupona haraka ili warejee majumbani kwao kuungana na familia zao katika shughuli za kila siku.
Posted by MROKI On Monday, July 04, 2016 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo