Nafasi Ya Matangazo

June 13, 2016

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maji safi na maji taka Dar es Salaam (DAWASCO), Cyprian Luhemeja akisaidiana na mafundi wa shirika hilo kufukua mabomba ya maji safi yanayovujisha maji katika mtaa wa Sinza E, Dar es Salaam jana. Dawasco imefanikiwa kudhitibi tatizo la upotevu wa maji kutoka asilimia 61 hadi 47 ya sasa
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maji safi na maji taka Dar es Salaam (DAWASCO), Cyprian Luhemeja (kulia) akiwaangalia mafundi wa shirika hilo waliokuwa wakifukua bomba la maji safi yanayovujisha maji katika mtaa Kasuku uliopo Sinza E, Dar es Salaam jana. Dawasco imefanikiwa kudhitibi tatizo la upotevu wa maji kutoka asilimia 61 hadi 47 ya sasa
 Mafundi wa Dawasco wakichimba bomba la maji safi kwaajili ya kuunganisha maji yaliyokuwa yameaktwa kwa muda mrefu baada ya mteja kushindwa kulipa bili.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maji safi na maji taka Dar es Salaam (DAWASCO), Cyprian Luhemeja (aliyesimama kushoto) akizungumza na mama mjane Asha Mohamed mkazi wa Mtaa wa Ngamia uliopo Sinza E, Dar es Salaam aliyekuwa amekatiwa maji tangu mwaka 2002 kwa kudaiwa sh 200,000 na jana Mkurugenzi huyo kuagiza arejeshewe maji na kuahidi kumlipia deni hilo mama huyo ili apate maji safi. Mama huyo aliahidi kuendelea kulipa bili hiyo ya maji. BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI.

*********************
SHIRIKA la majisafi na majitaka Dar es Salaam (DAWASCO), limefanikiwa kupunguza kiasi cha upotevu wa maji kutoka asilimia 61 hadi kufikia 47 huku ikiwa na mpango wa kufikisha asilimia 45 mwisho mwa mwezi juni.

Akizungumza wakati wa oparesheni maalumu ya kudhibiti mabomba ya maji yanayovujisha maji pamoja na kuwaunganishia maji wateja wake waliokatiwa maji kutokana na madeni Sinza Dar es Salaam jana, Afisa Mtendaji Mkuu wa Dawasco, Cyprian Luhemeja alisema wameamua kuingia mtaa hadi mtaa kukabiliana na tatizo hilo.

“Shirika limedhamiria kwa dhati kukabiliana na tatizo la upotevu wa maji, unaotokana na uchagavu wa miundombinu ambapo hadi sasa tumefanikiwa kupunguza tatizo hilo kutoka asilimia 61 ya awali hadi kufikia 47 ya sasa,” alisema Luhemeja.

Luhemeja alisema shirika limekuwa likiingia gharama kubwa ya kutibu maji kwa dawa lakini maji hayo yamekuwa yakiishia njia kutokana na uchakavu wa miundominu hivyo sasa wameamua kulivalia njuga tatizo hilo na kulimaliza kabisa.

Aidha mbali na udhibiti huo wa maji yanayovuja njiani pia Luhemeja alisema Dawasco imeamua kuwarejeshea wateja wake waliokatiwa maji kutokana na madeni ya muda mrefu na kukubaliana namna ya kulipa madeni hayo huku wakiendelea kupata huduma.

“Tunawateja wengi ambao walikatiwa maji kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na madeni tunawataka waje katika ofisi zetu za kanda zilizo karibu nao ili waweze kurejeshewa maji na kupangiwa utaratibu wa kulipa madeni yao,” alisema Luhemeja.

Wakiwa katika kazi hiyo ya kuunganishia watu maji na kutengeneza mabomba ya maji yanayovuja mtaa wa Sinza E Dar es Salaam, Afisa Mtendaji huyo alitoa ofa ya kumrejeshea huduma ya maji mama mjane Asha Mohamed mkazi wa Mtaa wa Ngamia, Sinza ambaye alikatiwa maji tangu mwaka 2002 kwa kudaiwa bili ya maji ya sh 200,000.

Akizungumza kwa furaha ya kurejeshewa maji Asha Mohamed, ameishukuru Dawasco kumrejeshea maji na kuahidi kulipa bili zake kwa wakati.

Nae Mwenyekiti wa Mtaa huo wa Sinza E, Kassim Kabulluh, alisema eneo lake likuwa likikabiliwa na kero ya uvujishaji maji barabarani jambo ambalo lilikuwa likiharibu miundombinu ya barabara.
Posted by MROKI On Monday, June 13, 2016 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo