Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Rais wa Uganda Mhe Yoweri Kaguta Museveni wakiongea na wanahabari mara baada ya kukutana na kufanya mazungumzo kwenye Ikulu Ndogo ya Arusha jijini Arusha leo Machi 1, 2016 mara tu baada ya Kiongozi huyo wa Uganda kuwasili jijini humo kuhudhuria Mkutano wa 17 wa Kawaida wa Wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
************
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki, amekutana na kufanya Mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Uganda Mheshimiwa
Yoeri Kaguta Museveni, ambapo pamoja na mambo mengine wamekubaliana kujengwa
kwa bomba la kusafirisha mafuta kutoka Bandari ya Tanga nchini Tanzania hadi
nchini Uganda.
Rais Museveni amemtembelea
Rais Magufuli katika Ikulu ndogo ya Arusha leo jioni mara baada ya kuwasili
hapa nchini akitokea nchini Uganda, ambapo hapo kesho atahudhuria Mkutano Mkuu wa
17 wa kawaida wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,
utakaofanyika katika Hoteli ya Ngurudoto Jijini Arusha.
Akizungumza baada ya viongozi
hao kufanya mazungumzo ya faragha, Rais Magufuli amesema wamekubaliana
kutekeleza mradi huo wa bomba la kusafirisha mafuta kutoka Tanga hadi Uganda,
kwa manufaa ya nchi zote mbili na nchi nyingine za Afrika Mashariki.
Amesema bomba hilo litakuwa na
urefu wa kilometa 1,120 na kwamba mradi huo utazalisha ajira za watu zaidi ya 15,000.
Rais Magufuli ameongeza kuwa
pamoja na kujengwa kwa bomba la mafuta, pia wamezungumzia kuongeza biashara
ndani ya nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki, kujenga viwanda na kuzalisha
ajira zaidi kupitia sekta mbalimbali za uzalishaji mali.
Aidha, Rais Magufuli amesema
katika Mkutano huu nchi wanachama watajadili maombi ya nchi ya Sudan Kusini
kupata uanachama ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Amebainisha kuwa, kwa Sudan
Kusini kuwa mwanachama Jumuiya ya Afrika Mashariki, itakuwa na uwezo wa kufanya
biashara katika eneo lenye takribani watu milioni 150 na hivyo kupata manufaa
makubwa zaidi.
Kwa upande wake Rais Yoeri Kaguta
Museven pamoja na kuunga mkono yaliyosemwa na Rais Magufuli amempongeza kwa
kasi yake nzuri aliyoanza nayo katika uongozi, na amesema ni matumaini yake kuwa
nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, sasa zitakuwa katika nafasi
nzuri ya kwenda kwa kasi ya Rais Magufuli katika maendeleo.
0 comments:
Post a Comment