Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akikagua CV za wafanyakazi wa Benki Kuu ya Tanzania alizoendazo wakati wa ziara yake ya kushtukiza jijini Dar es Salaam. Kulia kwake ni Gavana wa Benki Kuu Beno Ndulu.
***************
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
amefanya ziara ya kushitukiza katika Benki Kuu ya Tanzania (BOT), ambapo pamoja
na mambo mengine ameiagiza Benki hiyo kusitisha mara moja ulipaji wa
malimbikizo ya malipo ambayo tayari yalishaidhinishwa (Ex-Checker) na badala
yake yarejeshwe Wizara ya fedha na Mipango kwa ajili ya kufanyiwa uhakiki.
Mpaka Rais Magufuli anatoa agizo hilo, Benki Kuu ya Tanzania ilikuwa
katika mchakato wa kufanya malipo ya shilingi Bilioni 925.6, ambazo Wizara ya
Fedha ilitoa idhini ya kufanyika malipo.
Akizungumza na watendaji wakuu wa Benki Kuu ya Tanzania waliojumuisha
Gavana, Naibu Magavana, Wakurugenzi na Mameneja, Rais Magufuli ametaka Wizara
ya Fedha ifanye upya uhakiki wa malipo hayo, ili kubaini kama walengwa walioidhinishwa
kulipwa wanastahili kulipwa ama vinginevyo.
Aidha, Dkt. Magufuli ameagiza Kitengo cha madeni ya nje ambacho awali
kilikuwa chini ya Benki Kuu na baadaye kikahamishiwa Wizara ya Fedha, kirejeshwe
Benki Kuu mara moja ili kuimarisha udhibiti wa ukopaji na ulipaji wa madeni.
Wakati huo huo, Rais Dkt. John Pombe Magufuli amemuagiza Gavana wa
Benki Kuu ya Tanzania Prof. Beno Ndulu kupitia upya orodha ya wafanyakazi wa
Benki hiyo, na kuwaondoa mara moja wale wote ambao hawana ulazima wa kuwa
wafanyakazi katika benki hiyo.
"Haiwezekani tukawa na kundi kubwa la wafanyakazi, wanalipwa
mishahara wakati hata kazi wanazofanya hazijulikani" Amesema Dkt.
Magufuli.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo wakati ambapo Benki Kuu ya Tanzania ina
wafanyakazi 1391.
0 comments:
Post a Comment