Kuna taarifa na ushawishi unaoendelea wa baadhi ya wanachama, Wafuasi wa Vyama vya Upinzani kutaka kufanya maandamano waliyoyaita yasiyo na kikomo.
Najua wananchi wa Dodoma wangependa kufahamu nini tamko au wito wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma kuhusu ushawishi huo ambao ni kinyume cha sheria na wenye lengo la kutaka kuvuruga amani.
Kwanza niseme hakuna maandamano yatakayoruhusiwa katika Mkoa wa Dodoma, yenye lengo la kupinga uchaguzi uliofanyika tarehe 25/10/2015.
Pili hayataruhusiwa kwa sababu kulingana na matamshi, maandalizi na uhamasishaji wake una viashiria vilivyo dhahiri kuwa lengo lake ni kuleta vurugu itakayopelekea kuvuruga amani.
Tatu kulingana na sheria, kanuni na taratibu za Uchaguzi kama kuna mwenye malalamiko yaliyodhahiri na ya msingi zipo njia za kufuata na siyo kufanya maandamano yasiyo na kikomo.
Nitoe wito kwa Wananchama, Wafuasi wa vyama hivyo na wananchi kwa ujumla kutojihusisha katika maandamano hayo kwani atakayefanya hivyo atakabiliwa na mkono wa dola kwa nguvu zote kwa mujibu wa Sheria za nchi na asitokee wa kulaumu kwani atakuwa amejitakia mwenyewe.
Mwisho Wananchi waendelee na shughuli zao za maendeleo kama kawaida kwani Jeshi la Polisi Dodoma limejiandaa ipasavyo kuwalinda wanao tii sheria bila shuruti na kukabiliana na watakao kaidi kutii sheria bila shuruti.
Imetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna
Msaidizi Mwandamizi wa Polisi - Misime D.A (SACP)
0 comments:
Post a Comment