Bodi
ya Wakurugenzi Watendaji wa Benki ya Dunia leo wameidhinisha mkopo wa
maendeleo
wa Dola za Marekani milioni 80 zinazolenga kuboresha utendaji katika
sekta binafsi ya Tanzania, ili kukuza wajibu wake katika kujenga ajira
nchini.
Kwa
zaidi ya miaka kumi iliyopita, uwekezaji wa sekta binafsi ulikuwa
umejikita zaidi katika sekta chache zinazokua kwa kasi, kama vile sekta
za madini, fedha, mawasiliano na uchukuzi, wakati
sekta zinazohitaji nguvu kazi nyingi kama vile kilimo na uzalishaji
viwandani zilikua kwa kiwango chini ya wastani wa uchumi (takribani
asilimia 7 mwaka 2014/15). Matokeo yake ni kwamba ajira hazikuongezeka
kwa kasi inayolingana na kukua kwa idadi ya watu
wanaoweza kufanya kazi.
“Maelfu ya vijana wanaingia katika soko la ajira kila mwaka na wanakuwa na ari na matumaini makubwa,” anasema
Bi. Bella Bird, Mkurugenzi wa Benki ya Dunia nchini. “Kujenga
ajira zenye tija ni kipaumbele kwa Tanzania, na ni sekta binafsi pekee
ndiyo inayoweza kuzalisha idadi ya ajira zinazotakiwa. Mageuzi ya sera
yanayofadhiliwa na mradi huu
yatasaidia kupunguza vikwazo vya kufanya biashara nchini, kuruhusu
sekta binafsi na ukuaji wa ajira.”
Kila
mwaka, takribani vijana 800,000 wanaingia katika soko la ajira, ambalo
linatarajiwa kukua kutoka watu milioni 20 leo hadi watu milioni 40
ifikapo mwaka 2030. Fursa za kazi zenye tija kwa
vijana hawa bado ni finyu, nyingi zikiwa katika sekta isiyo rasmi.
Mazingira
ya Kazi kwa ajili ya Shughuli za Sera ya Kuendeleza Ajira ni programu
ya kwanza katika mfulululizo wa programu tatu za shughuli za msaada wa
bajeti kwa Tanzania. Shughuli hii inajenga
juu ya programu inayoongozwa na serikali ya ‘Matokeo Makubwa Sasa’
(BRN), na inasaidia programu kadhaa za sera zinazolenga katika kuboresha
kwa ujumla ‘urahisi wa kufanya biashara’ na kuimarisha masoko ya
vipengele vikuu (nguvu kazi, ardhi na mtaji). Aidha,
shughuli hii inasaidia maboresho yanayolenga kuinua mazingira ya
biashara katika biashara ya kilimo na utalii, sekta mbili zinazotoa
ajira nyingi ambazo ni muhimu kwa Tanzania.
“Tunaunga mkono hatua madhubuti za kurahisisha maisha ya biashara,” anasema
Andrea Dall’Olio, Kiongozi wa Kikosi Kazi cha Benki ya Dunia. “Kwa
mfano, tuliainisha ada, ushuru na kodi zaidi ya 59 zinazotozwa kwenye
sekta ya utalii na wakala mbalimbali wa serikali. Orodha kamili inaweza
kupatikana katika tovuti ya Wizara ya
Maliasili na Utalii, na tunaendelea kufanya kazi na serikali kupunguza
kwa kiasi kikubwa idadi yao na athari zake kwenye biashara.”
Shughuli hii ya Kuendeleza Sera ya Ajira
imetayarishwa kwa pamoja na Shirika la JICA (Japan International
Cooperation Agency), ambalo limepanga kutoa fedha sambamba na Benki ya
Dunia.
0 comments:
Post a Comment