Nafasi Ya Matangazo

February 06, 2015

Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)  imewafungia kati ya mechi tatu na nane wachezaji Juma Nyoso wa Mbeya City  na Aggrey Morris wa Azam kutokana na makosa ya kinidhamu waliyoyafanya  wakiwa uwanjani.

Nyoso ambaye alilalamikiwa na TFF kwa kumfanyia vitendo vya udhalilishaji  mshambuliaji Elias Maguri wa Simba amefungiwa mechi nane za Ligi Kuu ya  Vodacom (VPL). Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Ibara ya 57 na Ibara ya  11 (f) ya Kanuni za Nidhamu za TFF Toleo la 2012.

  Akiwa mbele ya Kamati hiyo jana (Februari 5 mwaka huu) jijini Dar es  Salaam, Nyoso alikiri kufanya na kujutia kosa hilo, pia amemuomba radhi  mchezaji Maguri kwa kitendo hicho.

 Akisoma uamuzi huo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Wakili Jerome Msemwa  alisema kitendo kilichofanywa na Nyoso ni kosa kubwa, kudhalilisha utu wa  mtu, na ni mfano mbaya kwa watoto na jamii nzima ya mpira wa miguu.


 Naye Morris amefungiwa mechi tatu za VPL baada ya kutiwa hatiani kwa  kumpiga mshambuliaji Emmanuel Okwi wakati timu hizo zilipopambana kwenye  mechi ya ligi iliyochezwa Januari 25 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es  Salaam.

 Kabla ya kusoma uamuzi, Wakili Msemwa alisema mlalamikiwa Morris alikiri  kugongana na Okwi, kwa maelezo kuwa aliingia kwenye 'reli' ndiyo ukatokea  mgongano huo.

Kamati baada ya kupitia malalamiko ya klabu ya Simba, ripoti za Brain CT  scan kutoka Besta Diagnostic Centre na nyingine kutoka Taasisi ya Mifupa  Muhimbili (MOI), taarifa za madaktari zilionyesha Okwi aligongwa kichwani  akiwa anacheza mpira na kuzimia kwa dakika tano, pia mkanda wa video  uliowasilishwa na TFF imeona kulikuwa na kugongana kati ya wachezaji hao.

 Hivyo, Kamati ikamtia hatiani Morris kwa kutumia Ibara ya 48(1)(d) ya  Kanuni za Nidhamu za TFF Toleo la 2012 kwa kumfungia mechi hizo tatu na  kumpa onyo kali.

 WAKATI HUO HUO Kamati hiyo imemfungia miezi sita na kumpiga faini ya sh. 200,000  Meneja Vifaa (Kit Manager) wa timu ya Polisi Mara, Clement Kajeri kwa  kuhamamisha vurugu na kuwapiga waamuzi kwenye mechi dhidi ya Mwadui  iliyochezwa Uwanja wa Karume mjini Musoma. Adhabu hiyo imetolewa kwa  kuzingatia kanuni ya 40(2) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Wachezaji watatu wa Friends Rangers; Mahmoud Othman, Khalid Twahil na John Alexander wamefungia miezi sita na faini ya sh. 500,000 kila mmoja kwa  kumpiga mwamuzi kwenye mechi ya Ligi Daraja la Kwanza dhidi ya Majimaji.

 Licha ya wachezaji hao kuitikia mwito wa Kamati, wachezaji hao walizuiwa na  viongozi wa kuingia ukumbini wakati malalamiko dhidi yao yalipoanza  kusikilizwa. Hatua hiyo iliifanya Kamati ifanye uamuzi baada ya kuusikiliza  upande wa walalamikaji pekee.

 Shauri dhidi ya mchezaji George Michael wa Ruvu Shooting kwa kumchezea  ubabe Amisi Tambwe wa Yanga, Kamati imeliahirisha baada ya mlalamikiwa  kupata udhuru uliosababisha asiwepo.

 Pia Kamati ya Nidhamu imeelekeza malalamiko ya timu ya Friends  Rangers  kupinga refa kuchezesha mechi yao dhidi ya Majimaji kwenye mvua kubwa,  kutoa maamuzi yasiyo halali na kutokuwepo na ukweli kwenye ripoti ya  Kamishna yakasikilizwe na Bodi ya Ligi kwa vile si masuala ya kinidhamu.
Posted by MROKI On Friday, February 06, 2015 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo