Na Mtua Salira, EANA
Rais wa Mahakama ya Afrika ya
Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) Jaji Augostino Ramadhani alikutana mwishoni
mwa wiki na Rais Jakaya Kikwete, Ikulu, Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo
mengine walijadili namna ya kuongeza kasi ya ujenzi wa makao makuu ya mahakama
hiyo.
Tanzania kama mwenyeji wa mahakama hiyo, itajenga makao katika
eneo la Kisongo, nje kidogo ya jiji la Arusha. Imeelezwa kwamba serikali tayari
imekamilisha michoro ya ujenzi wa mahakama hiyo.
Hivi sasa mahakama hiyo inafanyakazi kutoka makao yake ya muda
yaliyopo ndani ya ofisi za makao makuu ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), eneo la
Burka jijini Arusha tangu 2007.
Rais Kikwete pia alipewa taarifa fupi za shughuli za mahakama hiyo
na kujadili namna ya kuboresha uelewa wa raia juu ya uwepo wa mahakama hiyo
barani Afrika, Shirika Huri la Habari la Afrika Mashariki (EANA) limenukuu
taarifa iliyotolewa na mahakama hiyo kwa vyombo vya habari.
Tangu makubaliano ya kanzishwa kwa mahakama hiyo zaidi ya miaka 17
iliyopita, ni nchi 28 tu kati 54 wananchama wa Umoja wa Afrika (AU) ndiyo
zilizoridhia mkataba wa kuanzishwa mahakama hiyo ambapo pia nchi saba
zimeruhusu watu binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali(NGOs) kufungua kesi
katika mahakama hiyo.
Mafanikio ya mahakama hiyo kama chombo cha kupigania haki za
binadamu unahitajika uungwaji mkono na nchi wananchama kwa kuridhia uwepo wake.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Umoja wa Wanasheria Afrika, Don Deya
anasema kuridhiwa kwa mkataba huo na nchi zote wanachama wa AU kutaiwezesha
mahakama hiyo kutekeleza majumu yake kwa ufanisi.
0 comments:
Post a Comment