Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeizuia timu ya
Polisi Mara kutumia Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma kwa mechi zake
za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kuanzia leo mpaka hapo itakapotangazwa
vinginevyo.
Uamuzi huo umechukuliwa kutokana na matukio ya vurugu na uvunjifu
wa amani ambayo yamekuwa yakitokea kwenye mechi za FDL zinazochezwa kwenye
uwanja huo, ikiwemo ile ya Jumamosi iliyopita dhidi ya Mwadui ya Shinyanga
ambapo waamuzi walipigwa.
Kamati zinazohusika zitakutakana hivi karibuni kupitia matukio
yote ya utovu wa nidhamu kwenye FDL, na hatua kali zitachukuliwa kwa wahusika
ikiwemo na viwanja ambavyo vimekuwa na sifa ya vurugu.
Vyama vya mpira wa miguu vya mikoa vina wajibu wa kutoa ulinzi wa
kutosha viwanjani wakati wa mechi.
RAUNDI YA PILI TAIFA CUP WANAWAKE JUMAMOSI
Mechi za kwanza za raundi ya pili ya mashindano ya Taifa ya mpira
wa miguu kwa wanawake (Taifa Cup Wanawake) zinachezwa wikiendi hii (Januari 17
mwaka huu) kwenye miji minane tofauti nchini.
Timu tisa zilizofuzu kutoka raundi ya kwanza baada ya mechi za
nyumbani na ugenini akiwemo mshindwa bora (best loser) zitaungana na Ilala, Kinondoni
na Temeke kucheza raundi ya pili. Mechi za marudiano za raundi hiyo zitachezwa
Januari 21 mwaka huu.
Hatua ya robo fainali itakayochezwa Januari 26 na 27 mwaka huu
pamoja na nusu fainali na fainali ya michuano hiyo inayodhaminiwa na Proin
Promotions itafanyikia jijini Dar es Salaam.
KOCHA
NOOIJ KUTAJA STARS MABORESHO
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Mart Nooij anatarajia kutaja kikosi cha
Maboresho kitakachoingia kambini Januari 18 mwaka huu kujiandaa kwa mechi ya
kirafiki dhidi ya Rwanda itakayofanyika Januari 22 mwaka huu jijini Mwanza.
Nooij atataja kikosi hicho kwenye mkutano na waandishi wa habari
utakaofanyika kesho (Januari 15 mwaka huu) saa 5 asubuhi kwenye ofisi za
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Uwanja wa Karume.
0 comments:
Post a Comment