Polisi Mkoa wa Dodoma inawashikilia wanafunzi
84 wa chuo Kikuu UDOM kwa tuhuma za kuhamasisha uvunjifu wa amani Chuoni na
kufanya maandamano haramu kutoka Chuoni kuelekea katika Ofisi mbalimbali za
viongozi wa Serikali zilizopo Dodoma Mjini leo tarehe 14.01.2015 majira ya
05:30 (kumi na moja alfajiri).
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi David Misime – (SACP) ameeleza kuwa
chanzo cha wananfunzi hao wa programu maalum ya diploma ya Ualimu kufanya
uhalifu huo ni kikao walichofanya wananfunzi hao tarehe 13.01.201 wakidai
kuongezewa posho ya chakula na kwamba hata kiasi ambacho wanapewa wamechelewa
kupewa.
Hata hivyo uongozi wa Chuo uliwaeleza
kuwa wenye mamlaka ya kuzungumzia swala la kuongezewa posho ni Bodi ya Mikopo
na siyo chuo. Hivyo walitakiwa kufuata taratibu za kuwasilisha madai yao. Pia
walielezwa kuwa hundi kwa ajili ya fedha za posho zao zimeshasainiwa na
kuwasilishwa Benki ili waweze kuanza kupewa posho zao.
Hata hivyo wanafunzi hao hawakuridhika na usiku wakaanza kuhamasishana
kufanya maandamano jambo ambalo ni kosa kisheria. Wanafunzi hao wamehojiwa
kulingana na ushahidi ambao umekusanywa na wamefikishwa mahakamani kwa kosa la
Kufanya Maandamano yasiyo na kibali. Viongozi waliohamasisha uvunjifu huo wa
sheria baadi wamekamatwa na baadhi wanaendelea kutafutwa ili nao waweze
kuchukuliwa hatua stahiki. Ushahidi uliokusanywa unaonyesha jinsi viongozi hao
wameshiriki kuhamasisha kupitia vikao rasmi na visivyo rasmi, katika vikundi,
kupita katika mabweni na kutuma sms.
Kamanda wa Polisi ametoa wito kwa
Wanafunzi hao kutumia taratibu zilizowekwa na Serikali na Chuo kuwasilisha
malalamiko yao ngazi kwa ngazi na siyo kufanya vitendo vya kuvunja sheria ambavyo
vitawasababishia kukamatwa. Endapo watafanya hivyo wasije kulaumu mtu kwani
hatua zitachukuliwa kulingana na Sheria inavyoelekeza ikiwa ni pamoja na
kufikishwa mahakamani.
Imetolewa na Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Dodoma.
0 comments:
Post a Comment