Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeongeza
kwa siku kumi muda wa kumalizika usajili wa wachezaji wa klabu za Ligi Kuu ya
Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kutokana na kuchelewa kwa link ya mfumo mpya
wa usajili (system) kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Kwa mujibu wa CAF, link hiyo itakuwa tayari kwa
matumizi ndani ya siku tatu zijazo kutokana sasa. Hivyo, mameneja wa usajili wa
timu hizo kwa sasa wanatakiwa kukamilisha nyaraka zote zinazotakiwa ili link
hiyo itakapokuwa tayari waweze kuingiza usajili wao mara moja.
Kuanzia msimu wa 2014/2015 mfumo unaotumika kwa
usajili kwa klabu hizo ni wa elektroniki badala ya ule wa zamani wa kutumia
fomu za kawaida. Mfumo huo wa kisasa ambao pia unatumiwa na CAF unaondoa
upungufu uliokuwepo katika mfumo wa zamani.
Kutokana na mabadiliko hayo, usajili sasa utamalizika
Agosti 27 mwaka huu badala ya leo (Agosti 17 mwaka huu). Kipindi cha pingamizi
ni kuanzia Agosti 28 mwaka huu hadi Septemba 3 mwaka huu.
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji itakutana kati
ya Septemba 6 na 8 mwaka huu kwa ajili ya kupitia pingamizi na kuthibitisha
usajili.
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inayoshirikisha timu 14
itaanza Septemba 20 mwaka huu wakati ratiba inatarajia kutoka mwezi mmoja kabla
ya kuanza ligi hiyo. Ligi Daraja la Kwanza inatarajia kuanza wiki ya kwanza ya
Oktoba.
Mwisho wa kuombewa Hati ya Uhamisho ya Kimataifa (ITC)
kwa wachezaji wanatoka nje ya Tanzania ni Septemba 6 mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment