Nafasi Ya Matangazo

November 08, 2013

Ndugu zangu,
Jana saa kumi jioni nilishachukua nafasi yangu kwenye kijiwe hicho ( Pichani) cha wafanyabiashara ndogo ndogo Soko Kuu, Iringa.


Kwa kawaida, ndani ya banda hili la biashara kwa muda kama ule wa jana, watu huwa bize kuangalia mechi za Ligi Kuu zinazorushwa na Azam TV kutokea Dar. Na jana kulikuwa na Big Match; Azam dhidi ya Mbeya City.


Lakini, kwa umuhimu wa hotuba ya Rais, hata wapenzi wale wa soka waliamua kwa hiyari yao kusamehe soka na kubaki na hamu ya kufuatilia mambo muhimu kwa nchi, na kwa wakati huu.


Na hakika, aliyoanza nayo JK kwenye hotuba yake ndio haswa ilikuwa hamu ya Watanzania hawa niliojumuika nao kumsikiliza Rais wa Nchi.


Walikuwa na hamu sana ya kupata mtazamo na ufafanuzi wa Rais wao juu ya yaliyo karibu sana nao ( Proximity): Katiba na wimbi la Ujangili.  Katiba inahusu mustakabali wao na watoto wao. Inahusu pia ulinzi wa rasilimali zao. Kwamba Katiba iliyo bora inaweza pia kuwazuia ' Majangili wa Kisiasa' kuingia au kubaki madarakani huku wakifanya ' ujangili' wa mali ya umma  wakilindwa na mfumo dhaifu unaotokana na Katiba dhaifu.


Na Wananchi wale wanajua pia, kuwa wimbi la ujangili dhidi ya wanyamapori wetu unawahusisha pia vigogo wakiwemo wanasiasa. Wanataka kujua namna gani wahusika watadhibitiwa ili wasije kuwamaliza wanyamapori wetu kwa ' Ujangili' wao.


Suala la Afrika Mashariki na kutengwa kwa nchi yetu linawagusa na kuwakera Watanzania wengi. Wamefurahi kuwa Rais wa Nchi kalizungumzia Bungeni. Kwamba msimamo wetu kama nchi hatujitoi Afrika Mashariki.


Na ni ukweli, kuwa si ni Wana Jumuiya ya Afrika Mashariki na tutabaki kuwa hivyo. Hatuwezi kuwa jumuiya ya watu wa Afrika Magharibi, Kusini au Kaskazini.


Rais ameahidi kuendelea kuzungumza na Marais wenzake na tunaamini kuwa itafika mahali wenzake nao watatambua, kuwa hakuna Afrika Mashariki bila Tanzania.


Lakini, kwa Watanzania , Jumuiya ya Afrika Mashariki haiwaumizi sana kichwa kuliko haya ya Katiba , ujangili na mengineyo wanayokutana nayo nje ya milango yao kila kukicha.  Mambo yenye kauthiri maisha yao ya kila siku.


Maana, tunajua, kuwa hakuna nchi ya Afrika Mashariki itakayotulazimisha tushirikiane kwenye tusilotaka kushirikiana. Tukiweka msimamo wetu kama taifa utabaki kuwa hivyo, hata waje na vifaru vya kivita, tutapigania msimamo wetu na tutashinda.


Na katika hili iko wazi, kuwa kwa sasa Watanzania hatutaki yaingizwe kwenye jumuiya masuala ya Uhamiaji, Ajira, Ardhi, Sarafu Moja na nchi yetu kuwa ndani ya Shirikisho la Kisiasa. Mengine yote tumesema sawa.


Na Tanzania haitakuwa nchi ya kwanza duniani kuchagua mambo ya kushirikiana kwenye jumuiya. Mfano hai ni kwenye Jumuiya ya Ulaya, nchi ya Norway ni mwanachama lakini haimo kwenye ushirikiano wa masuala ya Uhamiaji ( Schengen) Hivyo hivyo kwa Uingereza.


Kwenye Jumuiya hiyo hiyo ya Ulaya, Norway, Sweden na Uingereza hawamo kwenye kushirikiana kwenye sarafu moja ya Euro. Na kuna mifano mingine. Yote haya yanatokana na matakwa ya wananchi wa nchi hizo kupitia kura za maoni. Kwamba wananchi wa nchi hizo wamekuwa tayari kuwa kwenye Jumuiya ya Ulaya lakini kuna maeneo ambayo wamekataa kuyaingiza kwenye jumuiya.


Na sisi Watanzania tutakuwa watu wa ajabu sana, katika mazingira yetu ya sasa, tukakubali kuyaingiza kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki maeneo ya Uhamiaji, Ajira, Ardhi, Sarafu , na hata kuwa ndani ya Shirikisho la kisiasa.


Hivyo basi, kuhusu Afrika Mashariki, Watanzania tuko nyuma ya Rais wetu kimsimamo, na hatutasogea hata hatua moja.


Lakini, kuna ya kwetu ya kila kukicha na yenye kutuhusu na kutuathiri leo,  na yatawahusu na kuwaathiri watoto na wajukuu zetu kesho na kesho kutwa. 


Ni haya ya Katiba, Ujangili, kutunga sheria za kubana vyombo vya habari ilihali  uporaji na kujimilikisha maelfu ya  ardhi bila hata kuyatumia kunaofanywa hata na wanasiasa wetu kukiendelea.


Haya yana athari ya mbaya kwa mwananchi  kila kukicha na tuendelee kupambana nayo kwa kasi zaidi...
Posted by MROKI On Friday, November 08, 2013 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo