Nafasi Ya Matangazo

November 07, 2013

Ndugu zangu,
RAIS Jakaya Kikwete ataongea na Wananchi jioni ya leo kupitia hotuba yake ya Bungeni.

Ilitarajiwa, kuwa Rais angetua Dodoma na kuzungumza na Wabunge kabla ya Muswaada wa Sheria ya Mabadiliko ya Marekebisho ya Katiba kujadiliwa.

Kimsingi anwani ya inakoelekezwa hotuba ya JK leo jioni ni kwa Wabunge wa CCM ambao vumbi la mjadala wa upande mmoja lililopelekea wao kupitisha muswaada wa sheria ya marekebisho ya katiba bado halijatua.

Na Wahenga walinena; yalopita si ndwele. Na Tusonge Mbele. Na akiwa Bungeni leo,  JK ataongea zaidi kama 'Mwenyekiti wa Chama' aliyevaa koti la dola. Na kwa utamaduni na kihistoria, Mwenyekiti wa Chama Tawala ni mtu mwenye nguvu sana. Mwelekeo wa hotuba yake hutengeneza hatma ya jambo husika. Maana, mwisho wa yote, wajumbe hujiuliza wenyewe; Mwenyekiti anataka twende wapi?

Na jioni ya leo JK ataongea juu ya suala la Afrika Mashariki, ujangili, DRC na mengineyo, lakini, KUBWA kabisa linalosubiriwa ni mtazamo wake  kuhusu KATIBA na njia anayoona inafaa tuenende nayo kama taifa.

Ndio, Watanzania wameshafahamu, kuwa KATIBA inahusu mustakabali wa nchi na vizazi vijavyo. Ni zaidi ya vyama vya siasa na majina ya wanasiasa waliopo.

Ni bahati njema kwa Watanzania, kuwa tuna Rais ambaye anaamini katika hilo. Na hakika, kwa JK kwenye hili la Katiba ana mawili ya kuchagua; Ama achague Chama Cha Mapinduzi, na hivyo yeye kuingizwa katika vitabu vya historia kama Mtanzania aliyepata kuwa Rais na akawa kama wengine, au kuchagua Umma, na hivyo kuchagua Mustakabali na yeye kuingizwa katika vitabu vya historia kama Rais aliyefungua ukurasa mpya kwa taifa la Tanzania. 

Na hatimaye, kuwa naye akawa mmoja wa watakaojadiliwa kwenye majopo yatakayotoa tuzo mbali mbali kwa wakuu wa nchi za dunia waliofanikisha mabadiliko ya kimsingi kwa watu wao.

Naam, yumkini hotuba ya JK jioni ya leo ikawa ya kihistoria. Kwa nafasi yake, hekima, busara na uwezo wa ushawishi alio nao, njia ya JK atakayoionyesha leo itafuatwa na Wabunge wengi wa chama chake, na hivyo, kumsaidia Rais na Mwenyekiti wao kutimiza azma yake ya kuwezesha uwepo wa Katiba itakayotokana na Wananchi, na hivyo, kuivusha nchi hii kutoka hapa ilipo na kusonga mbele zaidi.

Na kwa Waheshimiwa Wabunge wetu,  huu ni wakati wa kuongozwa zaidi na hekima na busara kuliko hisia na ushabiki na hususan wenye sura za vyama na kuangalia maslahi ya muda mfupi na ya kibinafsi zaidi.

Ikumbukwe, kuwa Rais wa Nchi anaongoza watu, na si mawe. Msingi wa kukubalika kisiasa ni lazima utokane na kukubalika na watu. Na hata hao wanaoitwa wapinzani kisiasa,  pia nyuma yao si mawe yaliyojipanga. Ni watu. Hivyo basi, inahusu watu. Inahusu Wananchi. Katiba ni mkataba baina ya watu katika jamii. Si miti na mawe.

Hivyo, ni muhimu sana watu kwa maana ya wananchi wakasikilizwa. Kama kuna manung'uniko yatafutiwe majawabu ili tufike salama kwenye kulifikia lengo kuu; Katiba ya Wananchi. Si ya chama tawala wala vyama vya upinzani. Ni jambo litakalotupeleka hata miaka 100 ijayo.

Maisha yetu hapa duniani ni mafupi sana. Wengi wetu hatutakuwepo, hata pale nchi yetu itakapotimiza miaka 100 ya Uhuru. Desemba 9, 2061.

Kila la kheri Rais Jakaya Kikwete  kwenye hotuba yako muhimu kwa nchi yetu jioni ya leo.
Posted by MROKI On Thursday, November 07, 2013 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo