Na Craig Ferla , Mara
Kuokoa maisha ya maelfu ya mama zetu na watoto wetu
wachanga Tanzania inawezekana! Kwa pamoja tunaweza kabisa kubuni mbinu mpya za
kufanikisha yale ambayo awali tuliyaona kama hayawezekaniki… Hivi sasa
ninapoandika makala hii, benki ya damu ya Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS)
Kanda ya Ziwa imefurika, huku maandalizi ya kuongeza uwezo wa taasisi hii
kupokea damu nyingi kwa mpigo yakiendelea, na hii ni kutokana na mwitikio
mkubwa wa wakazi wa wilaya zote za mkoa wa Mara kujitokeza kwa makundi makubwa
kujitolea damu kwa hiari! Mwitikio huo wa shamra shamra za maadhimisho ya Siku
ya Mchangiaji Damu Duniani ambayo kitaifa yanafanyika Mkoani Mara bila shaka
yoyote, umetokana na ujumbe wa wahamasisha jamii, kuwashawishi wakazi wa Mara
kutoa‘zawadi ya maisha,’hasa hasa ili kuokoa akina mama na
watoto.
Mama
Ye!ni kampeni
inayohimiza wanajamii kuchukua hatua kuokoa maisha ya maelfu ya mama zetu na
watoto wachanga wa Tanzania. Hii ni kampeni inayoongeza msisitizo wa Kampeni ya
kimataifa ya Kupunguza Vifo vitokanavyo na Uzazi Barani Afrika (CARMMA) iliyozinduliwa Novemba 2011 na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Kikwete. Kwa pamoja tumeazimia kuona
kuwa ‘Mama asife wakati analeta uhai.’
Kuna ambao watajiuliza kuna uhusiano gani kati ya
uhai wa akina mama na uchangiaji damu, na ni kwa niniMama Ye!imeungana
na NBTS na mamlaka za Mkoa wa Mara kwa ajili ya maadhimisho ya mwaka huu ya Siku
ya Mchangia Damu Duniani? Kwa mtazamo wangu, jibu ni rahisi. Takwimu za
Tanzania kwa kutumia makadirio ya Shirika la Afya Duniani zinakadiria kuwa 80%
ya damu inayokusanywa hutumika kwa watoto pamoja na akina mama wenye matatizo
yatokanayo na ujauzito.
Inakadiriwa kuwa kutokwa na damu nyingi baada ya
kujifungua ndicho chanzo kikuu cha vifo vya wanawake wajawazito, na
husababisha kifo kimoja kati ya kila vifo vitatu hadi vitano vya akina mama
wajawazito nchini Tanzania.
Aidha kuna uhaba mkubwa wa damu kwenye hospitali
zetu—huku ikikadiriwa kuwa ni theluthi moja tu ya chupa 450,000 za damu
zinazohitajika nchini kila mwaka ndizo zinazokusanywa. Ni wazi kabisa kuwa wapo
akina mama wetu wanaovuja damu nyingi baada ya kujifungua wanaofariki kutokana
na uhaba wa damu kwenye vituo vya tiba.
Iwapo watavuja damu nyingi baada ya
kujifungua, wanawake wanaweza kuhitaji kuongezewa damu ili kuwaokoa. Kama damu
itakuwepo katika vituo vya tiba, basi akina mama hao wataokolewa. Vile vile,
kama akina mama wengi wataokolewa basi watoto wachanga wengi nao wataokolewa,
na hii ni kutokana na uhusiano wa karibu kati ya uhai wa watoto wachanga na ule
wa mama zao.
Na la muhimu zaidi kwaMama Ye!– kuchangia
damu ni kitendo kinachobeba maana nzito na cha kuonekana, ambacho kinaweza
kufanywa na mtu yeyote yule ili kushiriki kuokoa maisha ya mama zetu. Ni
maamuzi yanayotokana na dhamira ya mtu kuchangia damu.
Na kama dhamira hiyo ya
kuchangia damu inatokana na nia ya kuokoa maisha ya akina mama, basi inaweza
kuwa chachu kwa mtu huyo huyo kuchukua hatua nyingine ambazo zinaweza kutendwa
na kila mtu ili kuwaokoa akina mama na watoto wetu wachanga.
Kwa mfano,
kuwahimiza akina mama wajawazito kuhudhuria kliniki japo mara nne; kuwawezesha
akina mama kujifungulia katika vituo vya tiba ambapo kuna mhudumu mwenye ujuzi
kwa kuwaandalia usafiri au kuwaangalia watoto wao pale nyumbani; na
kuwafuatilia viongozi katika jamii na kujua ni hatua gani zinachukuliwa kuhakikisha
uwepo wa huduma na ubora wa huduma hizo kwa akina mama na watoto wachanga.
Mara Oyee!!Mmetoa ujumbe wa kishindo katika wiki mbili
zilizopita, kutoa matumaini kwa uhai wa mama zetu na watoto wachanga!! NBTS
imethibitisha kuwa ukusanyaji wa damu katika sherehe za kitaifa kama hizi
umevuka kiwango kilichokuwa kimezoeleka!! Zaidi ya watu 1,250 wamechangia damu
katika sherehe za wilayani Bunda, Butiama, Serengeti, Tarime na Rorya wiki
iliyopita.
Wiki hii wakazi wa Manispaa ya Musoma nao pia wamejitokeza kwa
makundi makubwa—Jumla ya wakazi 500 wamechangia damu katika siku mbili tu
zilizopita, na wakati huo huo wakitoa ahadi zao na wito kwa wanajamii wengine
kuchukua hatua mbalimbali kuokoa maisha ya akina mama na watoto wachanga mkoani
Mara.
Na kwa hakika tangu maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Mchangiaji Damu
Dunani ya mwaka huu yaanze katikati ya Aprili, zaidi ya chupa 5,000 za damu
zimekusanywa mkoani Mara. Tembelea ukurasa wetu wafacebookkuona picha za jinsi Mkoa wa Mara ulivyoweka
historia mwaka huu katika shamra shamra za Siku ya Mchangiaji Damu Duniani,
nchini Tanzania!!
0 comments:
Post a Comment