Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na Mkuu wa jeshi la Polisi, Inspekta
Jenerali Said Mwema, ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam, wakati alipofika
kwa mazungumzo leo Mei 27, 2013.
****** ********
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal amekutana na Mkuu wa jeshi la
Polisi Inspekta Jenerali Said Mwema ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam
leo Jumatatu Mei 27, 2013.
Katika mkutano huo, Mheshimiwa
Makamu wa Rais ametumia nafasi hiyo kumpa pole Mkuu wa Polisi kufuatia ajali ya
gari la iliyosababisha vifo vya askari wanne wa Jeshi hilo, waliokuwa njiani
kutoka Nachingwea kuelekea Mkoani Mtwara kwa kazi maalum ya kudhibiti vurugu
zilizojitokeza Mkoani humo juma lililopita.
Mheshimiwa Makamu wa Rais
alisema, askari hao watazidi kukumbukwa kwa kuwa walikuwa mstari wa mbele
kuhakikisha majukumu yao kwa Taifa hili yanafanikiwa. Mheshimiwa Makamu wa Rais
alisema pia kuwa, serikali inathamini sana mchango wa Jeshi la Polisi sambamba
na majeshi mengine kutokana na kufanya kazi kwa kujitolea na kwa kutambua kuwa
ulinzi na usalama wa Taifa ni jambo muhimu kwa maendeleo ya nchi.
Mheshimiwa Makamu wa Rais
alimueleza Mkuu wa Polisi kuwa, kazi inayofanywa na jeshi lake ni kubwa na
kwamba Watanzania wanaithamini sana. Pia aliongeza kuwa katika nchi zote
wananchi wanaojitolea kufanya kazi katika vyombo vya usalama, ni miongoni mwa
wazalendo wakubwa wanaopaswa kuenziwa kwa kuwa wamekubali kuweka maisha yao kwa
ajili ya nchi na watu wake.
Katika
mkutano huo, Makamu wa Rais alitumia nafasi hiyo kupata taarifa kuhusu hali ya
usalama mkoani Mtwara na pia kubadilishana mawazo kuhusu kuhakikisha maeneo ya
nchi yetu kubakia salama wakati wote.
Na Boniphace Makene, Mwandishi
wa Habari wa Makamu wa Rais.
0 comments:
Post a Comment