TAARIFA KWA UMMA KUHUSU UTATUZI WA MGOGORO WA UONGOZI KATIKA CHAMA CHA SKAUTI TANZANIA
1.0 Chama Cha Skauti ni asasi isiyo ya kiserikali ambayo hutambulika kote duniani na mwanzilishi wake duniani ni Marehemu Lord Robert Baden Powell ambaye aliweza kuwaunganisha vijana wa rika mbali mbali duniani. Kwa Tanzania chama cha Skauti kilianza kutambulika katika medani ya kimataifa tokea mwaka 1963. Aidha chama cha Skauti Tanzania kwa sasa kinaendeshwa kwa mujibu wa katiba yake ya mwaka 1997.
Lengo kuu la Skauti ni kuwatayarisha vijana na kuwajenga katika maadili mema ili waweze kuwa waaminifu, wazalendo, rafiki wa wote, watiifu, wachangamfu, nwaangalifu na kuwa raia safi katika mawazo, maneno na vitendo.
Wanachama wa chama hiki wengi wao ni watoto na vijana kuanzia umri wa miaka 5-11 (Cubs), miaka 11-15 (Juniors), miaka 16-18 (Seniors) na miaka18-26 (Rovers). Wanachama walio katika umri huo wanakuwa bado wapo shuleni na vyuoni. Watu wazima (Adults) pia wanaweza kuwa wanachama wa Skauti kwa mujibu wa katiba.
Chama cha Skauti Tanzania kimekuwa na migogoro ya uongozi iliyosababisha kujenga makundi ndani ya chama. Migogoro hiyo imehusisha tuhuma mbalimbali zinazowakabili viongozi waliokuwa madarakani na hata waliomaliza muda wao. Baadhi ya tuhuma zimekuwa ni za kihistoria kwa kujirudia mara kwa mara, kama ifuatavyo:-
Tuhuma za Viongozi kujihusisha na biashara ya kusafirisha watu nje ya nchi, kujipatia fedha kinyume cha utaratibu, kujihusisha na biashara haramu ya madawa ya kulevya, kutumia madaraka vibaya na kugawa makundi ndani ya chama. Vitendo hivyo havistahili kuendelea ndani ya chama kinachotegemewa kustawisha jamii.
Ili kuondokana na tatizo hili, Chama cha Skauti hakina budi kuwa na viongozi bora na imara watakaoleta mababiliko chanya, na hivyo kurejesha imani kwa wanachama na jamii kwa ujumla. Moja ya suluhisho la kuondokana na migogoro hiyo ni kuwa na viongozi waadilifu watakaowajibika kusimamia vema chama kwa maslahi ya wanachama wote.
Kwa mujibu wa katiba ya chama hiki, uchaguzi mkuu ulipaswa kufanyika mwezi Juni mwaka 2010. Hata hivyo Baraza Kuu la Skauti katika kikao chake kilichofanyika Mwezi Januari 2010 Jijini Dar es salaam chini ya uongozi wa Makamu wa Rais wa Skauti Prof. Philemon Sarungi, liliazimia kuahirisha uchaguzi hadi mwaka 2011 kutokana na hali mbaya ya kifedha katika chama. Vilevile, iliamuliwa uchaguzi ufanyike mara baada ya uchaguzi Mkuu wa nchi, yaani ule wa Rais wa Nchi na Wabunge mwaka 2010 .
Katika Kuelekea kipindi cha uchaguzi, muhula wa uongozi wa Skauti Mkuu Tanzania ulimalizika mwezi Juni 2010. Kwa mujibu wa Katiba ya Skauti Tanzania (1997) kifungu cha 6.4 (c) majukumu ya Skauti Mkuu yalisimamiwa na Kamishna Mkuu Bw Lawrence Mhomwa tangu kipindi hicho.
2.0 Hali ya chama
Chini ya uongozi wa Kamishina Mkuu Lawrence Mhomwa, ambaye pia alikuwa na majukumu ya Skauti Mkuu, Chama kilipanga mkutano maalum uliofanyika tarehe 4 Februari 2011 mjini Bagamoyo. Uongozi uliokuwepo ulifanya maandalizi yote muhimu, ikiwa ni pamoja na mialiko na gharama za mkutano. Wajumbe wapatao 200 kutoka mikoani walihudhuria mkutano huo ambao ulikuwa na agenda kuu mbili :-
i Kupendekeza majina kwa ajili ya uteuzi wa nafasi ya Skauti Mkuu Tanzania.
ii Kupitisha mapendekezo ya marekebisho ya katiba ya chama cha Skauti Tanzania.
Kabla ya kufikia tarehe za mkutano, yalitokea malalamiko kutoka kwa wanachama wa Skauti ambao walidai kutotendewa haki katika mchakato mzima wa kupata wagombea. Baadhi yao walikimbilia mahakamani kuzuia mkutano usifanyike. Pia wajumbe wengine kutoka mikoani walizuiwa kuhudhuria kikao kwa madai kuwa hawakuwa wajumbe halali wa mkutano huo. Aidha, shutuma nyingi ziliwaelemea viongozi waliokuwa madarakani na wale waliomaliza muda wao, na hivyo kusababisha makundi ndani ya chama.
Ilionekana wazi kuwa, endapo agenda ya uchaguzi ungefanyika hali ya amani ndani ya chama ingetoweka kutokana na mvutano ulioanza kushika kasi baina ya makundi yaliyojitokeza.
3.0 Hatua zilizochukuliwa na Rais wa Skauti mwaka 2011:
Katika mazingira yaliyoainishwa hapo juu na kwa madaraka niliyonayo chini ya kifungu cha 6.3 (c) (ii) na (iv) cha Katiba tarehe 3/02/2011 nilimwandikia barua Kamishna Mkuu wa Skauti kumuelekeza kusitisha agenda ya uchaguzi wa Skauti Mkuu na kuendelea na mkutano kwa agenda ya Kupitisha mapendekezo ya marekebisho ya katiba ya chama.
Nilichukua uamuzi huo ili kuepusha fujo ambayo ingejitokeza kama uchaguzi ungefanyika. Ilihofiwa kuwa kundi lolote ambalo ‘kiongozi’ wake asingechaguliwa lingeanzisha fujo, hivyo tangazo la kusimamisha uchaguzi wa Skauti Mkuu lilitolewa na kutekelezwa kama nilivyoagiza. Wengine waliridhika na uamuzi huo na wengine walilalamika. Hata hivyo wajumbe wa Mkutano walitawanyika kwa amani.
Nafahamu kuwa maamuzi niliyoyachukua hayakuwafurahisha baadhi ya wanachama wa Skauti hasa wagombea katika kipindi hicho, lakini nilifanya hivyo ili kuhakikisha kuwa tunajipanga upya katika mchakato wa kupata uongozi kwa utaratibu unaokubalika kwa mujibu wa katiba ya chama cha Skauti.
4.0 Hatua za Kutatua mgogoro mwaka 2012
Nikiwa Rais wa Chama nimefanya mambo kadhaa ili kutatua mgogoro huu kabla na hata baada ya Mkutano Maalum. Baadhi ya mambo hayo ni:-
· Kwa nyakati mbali mbali niliwaagiza maofisa wa Wizara kufanya mazungumzo na viongozi wa Chama na Wadau ili kupata taarifa muhimu na kutafuta muafaka katika shauri hili;
· Niliongea na Viongozi Waandamizi wa Chama mmoja mmoja juu ya suala hili kwa lengo la kushauriana;
· Nilifanya mazungumzo na Kamati Tendaji ya Chama na kuwapa fursa kutoa maoni na ushauri wao;
· Maofisa wa Wizara walihudhuria mahakamani Bagamoyo ambapo liliwekwa pingamizi la uchaguzi wa Skauti Mkuu, hata hivyo kesi hiyo baadae ilifutwa baada ya upande walalamikaji kutohudhuria mahakamani;
· Maofisa wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi wameendelea kufuatilia hali ilivyokuwa katika Chama na kutoa ushauri ipasavyo;
· Nimeshauriana na Wadhamini wa Chama cha Skauti Tanzania na kupata maoni na maelekezo yao.
5.0 Uamuzi wa kutatua mgogoro.
Katika hali ya migogoro kama hii, Katiba inaelekeza Rais wa Chama, kwa kushirikiana na Bodi ya Wadhamini wa chama kuwa na wajibu wa kutafuta ufumbuzi wa matatizo katika chama endapo yatajitokeza. Kwa utekelezaji nimechukua hatua zifuatazo.
Baada ya kushauriana na wadhamini wa chama kwa mujibu wa katiba kifungu 6.2.(e) (iii) cha katiba ya chama, tumefikia maamuzi yafuatayo :- kuwa ni vema kuwa na safu mpya ya uongozi itakayopatikana kwa njia ya uchaguzi huru na wa haki. Kwa kuwa muda wa uongozi wa viongozi na Kamati Tendaji ya chama umelazimika toka mwezi Februari mwaka 2011, nimelazimika kuteua kamati ya muda yenye wajumbe 7 itayokuwa na jukumu kuu la kuandaa mchakato wa uchaguzi. Kamati ya muda itakuwa na wajumbe wafuatao:-
1. Brigedia Jenerali Mstaafu Gerald A. Mkude
2. Padre D. Mhando
3. Bw. Abdallah Sakasa
4. Bw. Salum S. Salum
5. Bibi Tunu Temu
6. Alhaji Zulu Liana
7. Bw. Bashiry Shelimoh
Kamati itafanya kazi kwa mujibu wa hadidu za rejea watakazokabidhiwa,
5.1 Muda wa Kamati.
Kamati itafanya kazi kwa muda usiozidi miezi 6 kuanzia tarehe ya uteuzi. Aidha, ninamteua Brigedia Jenerali Mstaafu Gerald A. Mkude kuwa Mwenyekiti wa kamati ya muda ili aongoze kamati hii kutekeleza majukumu waliyopewa.
Kwa taarifa hii nautaka uongozi uliositishwa kuiruhusu kamati ya muda kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Uongozi unaotakiwa kuachia madaraka ni Kamishna Mkuu ambaye pia ni Skauti Mkuu, Naibu Kamishna Mkuu, Kaimu Makamu Makamishna Wasaidizi wote na Wajumbe wote wa Kamati Tendaji Taifa (National Executive Commitee).
6.0 Hitimisho
Chama cha Skauti hakina budi kuwa na uongozi imara unaoweza kusimamia maadili ya vijana wetu hapa nchini . Hiki ni chama chenye historia ndefu chenye lengo la kuwaunganisha na kuwatayarisha vijana kuishi maisha ya kujiamini, kujituma na pia kusaidia wakati wote kunapotokea tatizo la kijamii. Tunataka tuwe na viongozi watakaotekeleza majukumu hayo na hatimaye kujenga mshikamano miongoni mwa vijana wa kitanzania. Ni matumaini yangu kuwa wale walioachia madaraka wataendelea kuwa Skauti bora, waadilifu na wenye ushirikiano kwa ajili ya manufaa ya chama
Ninatoa wito kwa wadau wote wa chama cha Skauti Tanzania, kupitia vikao halali vya chama katika kila ngazi kutoa ushirikiano kwa kamati ya muda ili kuhakikisha kuwa haki ya kidemokrasia inatendeka katika kupata safu mpya ya uongozi wa juu wa chama.
Asanteni kwa kunisikiliza
Dkt. Shukuru Jumanne Kawambwa (Mb).
RAIS WA CHAMA CHA SKAUTI TANZANIA
na
WAZIRI WA ELIMU NA MAFUNZO NA UFUNDI
0 comments:
Post a Comment