Nafasi Ya Matangazo

September 14, 2012

Na Father Kidevu Blog, Kinyenze-Mvomero
 MTU mmoja amefariki dunia na mwingine kujeruhiwa vibaya baada ya kufukiwa na kifusi katika machimbo ya kokoto yaliyopo Kitongoji cha Kinyenze, Kijiji cha Kipera Kata na Tarafa ya Mlali wilayani Mvomero mkoani Morogoro Septemba 11, 2012.

Kijana huyo aliyefariki ametajwa kuwa ni Rajabu Magunda huku aliyejeruhiwa ni Ramadhani Kiwaula ambao wawili hao walitajwa kuwa ni ndugu.

Akisimulia tukio hilo mmoja wa wakazi wa Kitongoji cha Kinyenze, ambaye pia ni mpasua kokoto katika machimbo ya Mlongaheka , Hamza Chamtu amesema ajali hiyo ilitokea majira ya mchana wakati marehemu alipofika mgodini hapo kumpa taarifa mdogo wake juu ya mama yao ambaye ni mgojwa.

“Mashimo yetu yapo jirani, marehemu nae huwa anachimba kokoto hapo lakini siku ya tukio yeye hupumzika na alikuja kumwambia mdogo wake juu ya habari za mgonjwa, lakini ndo wakati wanaongea wakiwa wamekaa katika ngema ndani ya shimo likawafunika na Rajabu kupoteza maisha, alisema Chamtu.

Anasema kuwa Ramadhani aligoma kwenda kumwona mama yake licha ya kujulishwa siku nyingi kuwa anaumwa na siku hiyo Marehemu alifika kumtaka ndugu yake huyo akamuone mama yake na aondoe tofauti zao.

“Marehemu kama alienda kumpatanisha na kumsihi akamjulie hali Bi mkubwa wao kabla hajafa maana hali yake ni mbaya, lakini ndo hivyo mauti yakamfika,” alisema Mkazi mwingine wa Kinyenze.

Ramadhani anadaiwa kujeruhiwa vibaya sehemu mbalimbali za mwili lakini majeraha zaidi yapo kichwani na kutenguka kiuno, kwani aliangukia katika jabali na kufunikwa na kifusi cha mawe hali yake sio nzuri na alikimbizwa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro ambako pia alihamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.

Hata hivyo wakati Septemba 12 watu wakijiandaa na maziko ya Rajabu, mama yao aliyekuwa mgonjwa nae alifariki na kuifanya familia hiyo kuwa katika misiba miwili.

Kitongoji cha Kinyenze kina machimbo manne ya Kokoto na mawe ya Mlongaheka, Sumo, Lugono na Kinyenze Umasaini.

Hii ni ajali ya pili kutokea katika machimbo hayo na kusababisho kifo baada ya mwaka juzi Sadick Makumbo kufukiwa na kifusi na kupoteza maisha.
Posted by MROKI On Friday, September 14, 2012 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo