Msaidizi wa mbunge wa jimbo la Singida mjini na katibu mwenezi wa CCM manispaa ya Singida Bw. Hassan Mazala (kulia), akimkabidhi Afisa wa idara wa shule za sekondari jimbo la Singida mjini Bw. David Bulala jezi 300 zilizotolewa na mbunge wa jimbo la Singida mjini Mh. Mohammed Gullam Dewji. Wa kwanza kushoto ni katibu muhtasi wa Mbunge.
Msaidizi wa mbunge wa jimbo la Singida mjini Bw. Hassan Mazala akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi jezi 300 kwa shule za sekondari za jimbo la Singida mjini. Wa pili kulia ni Afisa wa shule za sekondari jimbo la Singida mjini Bw. David Bulala na wa pili kushoto ni Katibu Muhtasi wa mbunge.
Baadhi ya jezi zilizotolewa msaada na mbunge wa jimbo la Singida mjini Mh. Mohammed Gullam Dewji kwa shule 20 za sekondari jimboni humo.
Na Nathaniel Limu
Mbunge wa jimbo la Singida mjini Mh. Mohammed Gullam Dewji ametoa msaada wa vifaa vya michezo jezi jozi 300, zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni sita kwa shule 20 za sekondari jimboni kwake.
Msaidizi wa mbunge huyo Bw. Hassan Mazala amesema hayo wakati akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi jezi hizo, iliyofanyika kwenye ofisi ya shirika lisilo la kiserikali la Saidia Singida yetu iliyopo mjini Singida.
Amesema jezi hizo zilikuwa ni sehemu ya msaada ambao ulikuwa utumike kwenye ligi maalum ya kombe la 'Mo' ambayo shule zote za sekondari jimbo la Singida mjini zingeshiriki.
"Lakini baada ya ninyi kuandaa bajeti kubwa mno na wakati huo huo mbunge wetu Dewji akikabiliwa na majukumu makubwa ya kutekeleza ahadi zake nyingi, ligi hiyo tumeisitisha kwanza",amesema Mazala ambaye pia ni katibu mwenezi wa CCM manispaa ya Singida.
Amesema kwa sababu ligi hiyo tarajiwa maandalizi yake bado, sasa maamuzi ni kwamba jezi hizo zitumike katika maandalizi ya michezo ya shule za sekondari (UMISETA).Akifafanua zaidi, Mazala amesema wanafunzi na vijana walio nje ya shule, wahamasishwe kupenda michezo ili pamoja na mambo mengine, waweze kujijengea mazingira mazuri ya kujiajiri na kuajiriwa.
Kwa upande wake Afisa elimu taalum shule za sekondari manispaa ya Singida Bw. David Bulala, alitumia fursa hiyo kumshukuru mbunge Dewji kwa kuipunguzia ofisi yake makali ya gharama ya ununuzi wa vifaa vya michezo.
0 comments:
Post a Comment