Nafasi Ya Matangazo

February 09, 2012

KATIKA hali isiyo ya kawaida, wabunge kutoka Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni leo wameiunga mkono Serikali iliyo madarakani na hata mmoja wao kudiriki kusema bungeni kuwa Mbunge atakayepinga mapendekezo ya Serikali katika Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ni muasi.

Msemaji wa Wizara ya Katiba na Sheria, Tundu Lissu amemsifu Rais Jakaya Kikwete kuwa amekuwa msikivu sana kwenye jambo hilo, na hakuangalia maslahi ya chama ila maslahi ya Taifa.


Amesema, Rais Kikwete amefanya kazi kubwa kushughulikia suala hilo , na kwamba kambi hiyo inaunga mkono mapendekezo ya Serikali.


Kambi hiyo imewaomba wabunge wote wamuunge mkono Rais ili kulipatia Taifa utaratibu wa kutengeneza Katiba mpya wenye mwafaka wa kitaifa.


“Mheshimiwa Spika, kwa mara ya kwanza, naomba kuunga mkono hoja hii” amesema Lissu bungeni mjini Dodoma na ameunga mkono mapendekezo yote ya Serikali kwenye muswada huo.


Spika wa Bunge alionesha kufurahishwa na kauli za Lissu na kuwaeleza wabunge kuwa, alivyofanya Mbunge huyo wa Singida Mashariki (Chadema), ndivyo inavyotakiwa.


Aliwataka wabunge waache chuki, hila na uhasama, wasibishane kwa misingi ya vyama, wabishane kwa hoja na kwamba, jambo hilo linamuhusu kila Mtanzania hivyo pia walijadili kwa makini.


“Huu muswa ni very tricky, hatujadili muswada wa mabadiliko ya Katiba, tunafanya amendments ya sheria iliyopo” amesema.


Makinda amewataka wabunge waujadili muswada huo wakiwa wamoja, na wananchi wajifunze kutoka kambi ya upinzani ili Watanzania wasonge mbele wakiwa na utulivu, umoja na upendo.


Wakati anatoa maoni yake kuhusu muswada huo, Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR- MAGEUZI) alimpongeza Rais kwa namna alivyoshughulikia muswada huo na akasema, wabunge watakaokataa mapendekezo ya Serikali ni waasi.


Baada ya kauli hiyo, Mbunge wa Viti Maalum, Anna Abdallah (CCM), aliomba mwongozo wa Spika akasema, lugha aliyoitumia Machali ni ya kuudhi hivyo afute kauli yake.


Alisema, si sahihi kuwaita wabunge hao waasi, na kwamba, kama ni uasi, waliuafanya wao mwaka jana, akimaanisha wabunge wa Chadema.


Spika wa Bunge alimtaka Machali afute kauli yake, Mbunge huyo alikubali kuifuta lakini akamtaka Anna Abdallah naye afute kauli yake kuwa wabunge wa Chadema waliasi mwaka jana.


Machali alifuta kauli yake lakini wakati anamalizia kuchangia alirudia maneno yale yale kwamba, “Na mtu yeyote atakayepinga hoja hii atakuwa muasi”.


Mbunge huyo pia alipinga kuli ya Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM) kuwa, wabunge wa Chadema hawakuwatendea haki Watanzania waliposusa na kutoka nje ya ukumbi wa Bunge wakati Bunge likijadili Muswada wa Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2011.


“Huu si muda wa kulalamika, kulalamika lalamika hakutusaidii” amesema Machali.


Chenge amewapongeza wabunge kutoka kambi ya upinzani kwa kutambua umuhimu wa Rais katika mchakato wa mabadiliko ya Katiba.
Source: Habarileo online. 
Posted by MROKI On Thursday, February 09, 2012 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo