Nafasi Ya Matangazo

October 30, 2011

Na Anna Nkinda- Perth Australia
30/10/2011 Wanawake  wametakiwa kutumia nafasi zinazotolewa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Wanawake (UNIFEM)  katika kujiletea maendeleo yao na ya mataifa yao kwani lengo kuu la kuanzishwa kwa shirika hilo ni kumuinua mwanamke na kuleta usawa wa kijinsia.

Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo Dk. Noeleen Heyzer wakati akiongea na wake wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuia ya Madola katika mkutano wao uliofanyika  Perth nchini Australia.

Dk. Heyzer alisema kuwa hivi sasa katika nchi nyingi Duniani wanawake wanapewa   nafasi za kupata elimu, kuwezeshwa  kiuchumi, usawa wa kijinsia , kupata afya bora kwa mama na mtoto na upatikanaji wa ajira hii yote ni kumfanya  mwanamke aweze kujiinua kiuchumi kwani hapo zamani wanawake walikuwa wameachwa nyuma kimaendeleo tofauti na wanaume.

“UNIFEM inashughulika na masuala ya usawa wa jinsia na uwezeshaji wa wanawake kiuchumi, kisiasa na kijamii hivyo basi ni jukumu lenu kuwahamasisha wanawake katika nchi mnazotoka ili waweze kuzitumia nafasi wanazopewa hii itawasaidia kujikwamua kiuchumi”, alisema

Baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa UNIFEM kumaliza kuongea na wake hao wa wakuu wan chi  akiwemo Mke wa Rais Mama Salma Kikwete walitembelea Halmashauri ya jiji la Perth upande wa Sekta ya Nishati na Madini na kuelezwa jinsi sekta hiyo ilivyochangia kutoa ajira na kuinua uchumi wa nchi hiyo.

Viongozi kutoka makampuni ya uchimbaji wa madini ambao ni Mtendaji Mkuu wa Chamber of Minerals and Energy of West Australia Reg Howard-Smith, Mkurugenzi Mtendaji  wa Argyle Diamonds Kevin McLeish na Josephine Archer ambaye ni meneja biashara kutoka Argyle Pink Diamonds walisema kuwa kutokana na jiografia nzuri mji huo umejaliwa kuwa na madini mengi ukilinganisha na miji mingine.
“Upande wa Magharibi wa Nchi yetu kuna miji minne ambayo ni Kimberley, Pilbara, Yilgarn na Kusini Magharibi ambako kunapatikana madini zaidi ya aina 50  baadhi yakiwa ni  dhahabu, almasi, chuma, mchanga mzito wenye madini aina tofauti, base metals, chumvi, chuma cha pua, Ilmenite, Rutile, Alumina, Zircon, Garnet na Tantaluma”, walisema.
 
 Wake wa wakuu wan chi wanachama wa Jumuia ya madola waliweza kujionea aina mbalimbali za madini yanayopatikana katika nchi hiyo pamoja na vito vya thamani na bidhaa zinazotengenezwa kutokana na madini hayo.
Aidha waliweza kutembelea bustani ya kutunza mimea na wanyama wa asili nakuona jinsi viumbe hai vya kale vinavyotunzwa ili visiweze kupotea  kwa ajili ya kumbukumbu ya vizazi vijavyo na wageni wanaotembelea nchi hiyo.
Mkutano wa  wakuu wa Nchi wanachama  ya Jumuia ya madola umemalizika leo na Kaulimbiu ya mwaka 2011 ya Jumuia hiyo  ni “Wanawake ni wakala wa mabadiliko”.
Posted by MROKI On Sunday, October 30, 2011 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo