Nafasi Ya Matangazo

February 04, 2011

Waziri wa Viwanda na Biashara Dr. Cyril Chami akizungumza na wanahabari (hawapo pichani)hii leo.

TAMKO LA WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA MHE DKT. CYRIL CHAMI KWA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU WAFANYABIASHARA WA KIGENI WANAOFANYA BIASHARA KINYUME CHA SHERIA KATIKA ENEO LA KARIAKOO

1.0 UTANGULIZI

Kuanzia mwaka 2009, Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Wizara pamoja na Taasisi nyingine za Serikali zimekuwa zikifuatilia kwa karibu uendeshaji wa shughuli za biashara katika eneo la Kariakoo. Juhudi za makusudi za Serikali za kushughulikia na kusimamia biashara eneo la Kariakoo zilitokana pamoja na mambo mengine, taarifa ya Kikosi Kazi kilichokuwa kimeundwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kufuatilia ushiriki wa raia wa kigeni katika biashara ndogo ndogo. Aidha, ukaguzi wa biashara zote mkoani Dar es Salaam ulifanywa na Wizara ya Viwanda na Biashara kuainisha changamoto mbali mbali zinazohusu utekelezaji wa sheria za biashara nchini. Changamoto hizo ziliwasilishwa kwenye Wizara na Taasisi husika kwa lengo la kufanyiwa kazi.

Kufuatia uteuzi wa Baraza la Mawaziri mwezi Novemba, 2010, Mhe. Waziri wa Viwanda na Biashara alitoa tamko kwa nyakati tofauti la kuwataka wafanyabiashara wote nchini ikiwa ni pamoja na wale wanaotoka nje ya nchi kufuata Sheria za nchi. Aidha, mnamo tarehe 06 Januari, 2011 katika azma ya kuimarisha utekelezaji wa mikakati ya kuboresha mazingira ya biashara nchini, Serikali ilitoa tamko la kuwataka wafanyabiashara wa kigeni wanaofanya biashara kinyume na vibali vyao vya kuishi nchini kuacha kujihusisha na biashara hizo na kuwapa siku thelathini kuhakikisha kuwa wanafuata sheria za nchi. Vilevile, Serikali ilibainisha kuwa wafanyabiashara watakaokaidi agizo hilo watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Katika hatua za kuendeleza utekelezaji wa mikakati ya kuboresha mazingira ya biashara hususan eneo la Kariakoo mwezi Januari, 2011, Wizara iliunda Kikosi Kazi chenye wajumbe kutoka Wizara na Taasisi mbalimbali zinazosimamia biashara nchini ili kufanya tathmini ya mwenendo wa biashara katika eneo hilo na kuandaa mapendekezo ya utekelezaji. Wajumbe wa kikosi kazi hicho walitoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Ofisi ya Waziri Mkuu-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Kazi na Ajira, Wizara ya Mambo ya Ndani, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Idara ya Uhamiaji. Kikosi Kazi hicho kiliaandaa mapendekezo ya kuboresha biashara katika eneo hilo na maeneo mengine kwa ujumla.

2.0 TATHMINI YA MWENENDO WA BIASHARA ENEO LA KARIAKOO

Uchambuzi uliofanywa na Kikosi Kazi, umebainisha mambo yafuatayo kuhusu biashara zinazofanywa katika eneo la Kariakoo:-

(i) Kariakoo imekuwa kiungo muhimu cha biashara kati ya Tanzania na Nchi inazopakana nazo kama Uganda, Rwanda, Burundi, Komoro, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Zambia, Malawi, Kenya na Msumbiji. Kutokana na umuhimu huo, eneo la Kariakoo linawavutia wafanya biashara kutoka nchi mbalimbali wanaonunua na kusafirisha bidhaa kwenda katika Nchi hizo;

(ii) Eneo la Kariakoo limeendelea kuwa kiungo muhimu cha biashara na mikoa mbalimbali Tanzania Bara na Visiwani (Zanzibar);

(iii) Hali ya miundombinu ya eneo la Kariakoo kama vile sehemu za kuegesha magari, huduma za kibenki, maeneo ya kuwakutanisha wafanyabiashara kwa lengo la kufanya majadiliano ya kibiashara, na mahitaji mengine haikidhi mahitaji ya biashara ya eneo hilo kwa sasa;

(iv) Bidhaa nyingi zilizopo Kariakoo zinazalishwa nchi za bara la Asia. Hivyo, kuna uhusiano mkubwa wa kibiashara kati ya Tanzania na nchi hizo;

(v) Ushindani wa biashara katika eneo la Kariakoo ni mkubwa kutokana na umuhimu wa eneo hilo kwa biashara za ndani na nje ya nchi. Hali hii imesababisha ongezeko la kodi ya pango na hivyo kusababisha wafanyabiashara wadogo kushindwa kumudu gharama ya pango na baadhi yao kuanza kutumia maeneo ya wazi kwa biashara zao;

(vi) Kuongozeka kwa wawekezaji na wafanyabiashara wa kigeni katika eneo la Kariakoo ni fursa kwa wafanyabiashara wa Tanzania kujifunza mbinu mbalimbali za biashara na kuwezesha matumizi ya teknolojia toka nje ili kuzalisha bidhaa na huduma bora na hivyo kuhimili ushindani;

(vii) Wafanyabiashara wadogo wanakabiliwa na changamoto za ukosefu wa elimu ya biashara na upatikanaji wa mitaji na hivyo kujikuta wanashindwa kuhimili ushindani wa biashara uliopo katika eneo la Kariakoo ambao umechukua sura ya kimataifa;

(viii) Sheria zinazosimamia uwekezaji na biashara nchini zinakidhi mahitaji ya jamii ya wafanyabiashara wa nje na ndani. Hata hivyo, ipo haja ya kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa Sheria za uwekezaji na biashara kwa wahusika wote ili kuhakikisha kuwa biashara zinafanyika kwa tija na kwa ushindani wa haki.

Kufuatia agizo la Serikali kupitia kwa viongozi mbalimbali kuhusu wageni na wananchi wote wanaojishughulisha na biashara kinyume cha sheria, baadhi ya wafanyabiashara wa kigeni waliokuwa wanafanya biashara za uchuuzi katika eneo la Kariakoo wameanza kufuata Sheria na Kanuni kwa mujibu wa vibali vyao vya biashara na uwekezaji. Serikali inapenda kuchukua fursa hii kuwapongeza wafanyabiashara wote wazalendo na wa kigeni wanaofanya shughuli zao kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi. Kuanzia sasa wafanyabiashara watakaokiuka taratibu za biashara wanazozifanya watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

3.0 MIKAKATI YA SERIKALI KUHUSU KUENDELEZA BIASHARA ENEO LA KARIAKOO

Ili kukabiliana na changamoto zilizojitokeza, Serikali imejipanga katika kuhakikisha kwamba biashara zinafanyika kwa tija, katika maeneo sahihi na kwa mujibu wa sheria za nchi yetu. Mikakati iliyowekwa kufanikisha azma hiyo ni kama ifuatavyo:-

3.1 Mipango ya muda mfupi

3.1.0 Kukamata wageni wote wamachinga kuanzia kesho tarehe 05 Februari 2011. Aidha, yeyote atakayemwona mmachinga wa kigeni atoe taarifa polisi kwa kutumia namba ---------

3.1.1 Kufanya ukaguzi wa kina katika maeneo yote ya biashara Jijini Dar es Salaam ili kuhakikisha kwamba wafanyabiashara wote wa kigeni na watanzania wanafanya biashara kwa mujibu wa sheria na vibali walivyopewa;

3.1.2 Serikali kuendelea kutoa mafunzo kwa wafanyabiashara hususan wajasiriamali wadogo kwa lengo la kuwawezesha kumudu ushindani. Kwa mfano, katika mwaka 2010, wajasiriamali waliofaidika na huduma za SIDO katika mkoa wa Dar es Salaam ni pamoja na wajasiriamali 615 waliopatiwa mikopo ya thamani ya shillingi millioni 514; wajasiriamali 1,053 waliopatiwa mafunzo; na vikundi 38 vilivyowezeshwa kujiunga pamoja. Aidha SIDO ilishirikina na Tanzania Private Sector Foundation kuendeleza wajasiriamali 372 waliopatiwa mitaji ya Shillingi 1.1 billioni.

3.1.3 Kuendelea kufanya ufuatiliaji wa wafanyabiashara wanaofanya biashara kinyume na taratibu na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria za nchi yetu;

3.1.4 Kusimamia wafanyabiashara kufanya shughuli zao katika maeneo yaliyoidhinishwa kwa biashara;

3.1.5 Kuhakikisha kila Taasisi inayohusika na usimamizi wa sheria za biashara inatenga fedha za kutosha kwa ajili ya ufuatiliaji na tathmini ya biashara; na

3.1.6 Kuhakikisha kuwa kunakuwa na Jukwaa (Platform) ya wadau wa masuala ya uwekezaji na biashara ambayo itakuwa na jukumu la kujadiliana na kufanya tathimini ya masuala hayo kila baada ya kipindi cha robo mwaka (Quarterly).

3.2 Mipango ya Muda Mrefu

3.2.1 Kujenga kituo cha biashara “logistic centre” kwa ajili ya kurahisisha uingizaji wa bidhaa toka nje ya nchi na kudhibiti ubora wa bidhaa hizo;

3.2.2 Kujenga Kituo cha Mauzo Nje “Re-export Centre” kwa ajili ya kurahisisha na kuwezesha biashara ya bidhaa za Tanzania na zile zinaingizwa toka nje kwa lengo la kuuzwa katika nchi jirani zinazotuzunguka;

3.2.3 Kuendelea kuboresha mazingira wezeshi ya biashara kwa ajili ya kuwavutia wawekezaji na wafanyabiashara nchini. Hii itawezesha kuongeza fursa za biashara, ajira na kukua kwa uchumi wa Tanzania.

3.2.4 Kutenga maeneo maalum kwa biashara za jumla ili Wafanyabiashara watanzania wanaofanya biashara za reja reja waende kununua bidhaa katika maduka ya jumla yatakayokuwa yametengewa maeneo maalum;

3.2.5 Kuboresha miundombinu ya eneo la Kariakoo na viunga vyake ili biashara ziweze kufanyika kwa ufanisi zaidi;

3.2.6 Kuandaa mkakati wa kuboresha maeneo mengine katika Manispaa za Temeke, Ilala na Kinondoni na kuondoa dhana iliyojengeka kwa wafanyabiashara kuwa Kariakoo ndiyo eneo pekee ambalo ni kivutio kwa biashara;

3.2.7 Kuandaa mfumo wa uhifadhi wa taarifa (database) za wafanyabiashara za aina zote ili kurahisisha ufuatiliaji, uchambuzi na tathmini ya aina ya biashara zinazofanyika nchini; na

3.2.8 Kufanya mapitio ya sheria ili kuboresha mwenendo wa biashara nchini.

Serikali inatambua umuhimu wa kuendeleza uwekezaji, uzalishaji na biashara ili kuongeza ajira na kipato kwa wananchi walio wengi. Hivyo, Serikali itaendelea kuwakaribisha wawekezaji wa ndani na wa nje kwa kwa lengo la kukuza uwekezaji na biashara nchini kulingana na sheria na Taratibu zilizopo.

Aidha, Serikali itaendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara na wawekezaji kuhusu utaratibu na sheria za nchi katika kufanya biashara.

WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA

04 FEBRUARI 2011

Posted by MROKI On Friday, February 04, 2011 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo