Full nondo
WATU zaidi ya 16 wamekufa papohapo katika ajali ya magari manne yaliyogongana katika daraja la mto Nduruma uliopo katika wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha.
Katika ajali hiyo iliyotokea saa 9 mchana leo (21-01-2009) , maiti tatu zimetambuliwa; ya Sista Anastazia wa Kanisa la Mtakatifu Fransisco lililopo Guruka Arusha, Mchungaji Maina Kileli raia wa Kenya na Alais Kinya mkazi wa Moshi.
Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo,Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha ,Basilio Matei alisema watu 16 walifariki hapo hapo na majeruhi 17 ambapo chanzo cha ajali hiyo ni kufeli kwa breki ya roli la Soda mali ya Kampuni ya Bonite lenye namba ya usajili T420 AMM.
Alisema roli hilo lililokuwa likishuka mteremkoni karibu na daraja liligonga kwa nyuma Coaster yenye namba T 799 AWR iliyokuwa mbele yake zote zikitokea Arusha kuelekea Moshi na kutumbukia mtoni.
Alisema Coster iliyokuwa na abiria ilibaki ikininginia katika vyuma vya daraja ambapo watu wengi walitumbukia mtoni huku magari mawili Randrover 109 yenye namba T 820 AMC na Hiace yenye namba T607 ANW zilizokuwa zikitokea Moshi kuelekea Arusha zilikutana na ajali hiyo na kugongwa na tera la roli lililokuwa limejaza machupa ya soda wakati wa kupishana.
Kamanda alisema maiti na majeruhi wako Hospitali ya Mount meru na wengine katika Hospitali na Kanisa la Kilutheri ya Seliana ambapo watu wamekatika vipande vipande na nyama zikiwa zimezagaa eneo la ajali.






0 comments:
Post a Comment