Nafasi Ya Matangazo

May 16, 2024

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango akisalimiana na Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Canada Mhe. Ahmed Hussein mara baada ya mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 16 Mei 2024.
Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Canada Mhe. Ahmed Hussein akizungumza jambo wakati wa mazungumzo hayo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango akifanya mazungumzo na Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Canada Mhe. Ahmed Hussein Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 16 Mei 2024.
Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Canada Mhe. Ahmed Hussein (kulia) na ujumbe wake wakiwa katika mazungumzo hayo na makamu wa Rais wa Tanzania. 
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Canada Mhe. Ahmed Hussein mara baada ya mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 16 Mei 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango akiagana na Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Canada Mhe. Ahmed Hussein mara baada ya mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 16 Mei 2024.
********
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Canada Mhe. Ahmed Hussen Ikulu Jijini Dar es Salaam.
 
Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais amesema Tanzania inathamini uhusiano wa kidiplomasia uliopo baina yake na Canada na kuishukuru kwa kuinguka mkono Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo Afya, Elimu, Biashara na Uwekezaji, Kilimo pamoja na Ulinzi na Usalama. Amesema Mataifa haya mawili yameendelea kushirikiana kimataifa ikiwemo Jumuiya ya Madola pamoja na Umoja wa Mataifa.
 
Makamu wa Rais ameikaribisha Canada kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha uchumi wa buluu kwa kutumia uzoefu wa nchi hiyo pamoja na kukaribisha wawekezaji katika sekta hiyo. Pia ameishukuru Serikali ya Canada kwa kuunga mkono ajenda ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya nishati safi ya kupikia. Amesema kuunga mkono jitihada hizo kutaharakisha wananchi wa Tanzania kuondokana na nishati isiyofaa ya kupikia na kufikia malengo ya mkakati wa kitaifa wa kufikia asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi ifikapo mwaka 2034.
 
Makamu wa Rais amesema kwa sasa Tanzania ni sehemu sahihi zaidi kuwekeza kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza katika kuimarisha uchumi pamoja na kuweka mazingira mazuri zaidi ya uwekezaji na biashara kwa kufanya mageuzi ya kitaasisi, kisera na kuimarisha utawala wa demokrasia. Amesema ni muhimu kufanya kazi pamoja katika kuharakisha majadiliano ya kuboresha Mkataba wenye usawa na maslahi kwa pande zote mbili wa kinga katika uwekezaji baina ya Canada na Tanzania (FIPA).
 
Aidha amesema Serikali ya Canada inaweza kushirikiana zaidi na Tanzania katika sekta ya afya kwa ujenzi wa viwanda vya kuzalisha dawa, kuwekeza katika makao makuu ya nchi Dodoma katika ujenzi wa miundombinu, udhibiti wa taka ngumu, viwanja vya michezo pamoja na mazao ya mbogamboga.
 
Vilevile Makamu wa Rais ameishukuru serikali ya Canada kwa kuiunga mkono Tanzania dozi milioni 22 za vitamini A pamoja na kutangaza ahadi ya dola milioni 25 katika mradi wa kilimo rafiki kwa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
 
Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Canada Mhe. Ahmed Hussen amesema uhusiano wa Tanzania na Canada ni wa muda mrefu katika hali zote ambao umeendelea kuimarika. Amesema katika wakati huu ambao Tanzania imefikia uchumi wa kati wa chini ni muda muafaka wa kuongeza ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili.
 
Amesema katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi Canada inatambua umuhimu wa kufanya kazi pamoja ili kuondoa athari kwa wananchi. Ametoa pole kwa serikali na wananchi wa Tanzania na familia zilizoathirika na kimbunga hidaya pamoja na mvua za el nino zilizopolekea madhara makubwa.
 
Ameongeza kwamba Canada inaendesha miradi mbalimbali nchini Tanzania ikiwemo ya kuwajengea uwezo wananchi katika kuhimili mabadiliko ya tabianchi pamoja na kilimo rafiki kwa mazingira.
 
Waziri Hussen amesema Canada itaendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo mazingira, afya, lishe na elimu.
Posted by MROKI On Thursday, May 16, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo